Sikia hii, Kama ulikuwa unadhani zile ‘Thank You’ walizopewa mastaa wa Yanga zimeshakamilika, basi utakuwa umekosea sana, kwani kuna jipya linatarajiwa kupitishwa tena na kocha mkuu mpya, Miguel Angel Gamondi kufyeka baadhi ya nyota watakaoshtua mashabiki wa klabu hiyo.
Kocha huyo kutoka Argentina anaonyesha hatanii kwani mipango yake ni kusuka kikosi cha kisasa zaidi na juzi amewashtua mabosi wa klabu yake akiwatangazia kwamba anataka kuona kikosi chake kinacheza soka la kisasa litakalohusisha mipango ya kisasa ya kuzuia, ila akili kubwa ni kushambulia.
Kwenye hesabu hizo ametaka kuletewa nguvu kubwa watu wa kushambulia na kufunga kuliko watu wazuiaji hatua ambayo hata usajili wa kiungo Jonas Mkude unaweza kuingia mashakani kukamilika.
Kocha huyo amebariki sababu za mastaa watano waliopewa ‘Thank You’, lakini akawaambia viongozi wake kwamba kuna wengine anataka kupishana nao mara tu baada ya kufika nchini.
Yanga hadi sasa imeshawatema kipa Erick Johola, mabeki Abdallah Shaibu ‘Ninja’, mawinga Tuisila Kisinda, Dickson Ambundo na mshambuliaji Bernard Morrison.
Gamondi amewaambia mabosi wa Yanga kuwa, hata usajili wa viungo wakabaji sio kitu muhimu kwake na kwamba anataja kuona watu bora wenye makali ya kutengeneza mashambulizi kwenda mbele na sio kuzuia.
Mwanaspoti linafahamu kama kuna beki mwenye maana ambaye amepitishwa haraka na Gamondi ni Joyce Lomalisa Mutambala ambaye amezuia Mkongomani huyu kuondoka akitaka amkute kwani anajua matumizi yake katika kikosi hicho.
“Tulimueleza Lomalisa anataka kuondoka, akaangalia jinsi alivyocheza msimu uliopita, akasema alikuwa anakosewa matumizi yake, akatuambia tumwambie abaki anakuja kufanya naye kazi,” alisema bosi huyo wa juu kabisa wa Yanga.
Bosi huyo aliongeza, kuna wachezaji wanaweza kuja kupoteza nafasi ndani ya timu hiyo kiasi cha kukatwa bila kujali mikataba yako huku Muargentina huyo akitaka kuona anabaki na watu bora kwenye kikosi chake
“Hivyo kuna watu zaidi wanaweza kuja kukatwa watakaoshtua lakini ndio kocha ametaka, anachotaka ni kuona anabaki na watu ambao watakuwa na namba nzuri za kumpa matokeo, ametuambia maamuzi yake hayataangalia jina la mchezaji, akitolea mfano mtu kama Mayele (Fiston) akisema ameridhishwa sana na kazi kubwa aliyoifanya.”