Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Februari 13, 2023 ameanza siara ya siku tatu mkoani Songwe ambapo anatarajiwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Waziri Majaliwa amewasili leo mkoani Songwe na kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Songwe na viongozi wa mkoa huo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba ambapo baada ya kuwasili ameondoka kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ambako amekagua na kuweka jiwe la msingi katika hospitali ya wilaya.
Kesho Februari 14, 2023 Waziri Mkuu atakagua Kiwanda cha kukoboa kahawa cha GDM katika Halmashauri ya Wilaya Mbozi na baadaye ataelekea katika Wilaya ya Momba ambako atakagua ujenzi wa soko la kimataifa la mazao la Kakozi na kisha atakwenda Halmashauri ya Mji Tunduma.