Serikali imesema asilimia 12.2 ya vijana wenye umri wa miaka 15-35 nchini Tanzania hawana ajira.
Asilimia hiyo ni sawa na vijana 1,732,509 kati ya nguvu kazi ya vijana 14, 219,191 wenye uwezo wa kufanya kazi kwa maana ya vijana walio katika umri huo na hawapo katika mafunzo au hawana ulemavu unaosababisha wasijishughulishe na shughuli za kiuchumi.
Takwimu hizo zimetolewa leo Februari 3, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Patrobas Katambi.
Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina (CCM) ambaye amehoji ni vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Naibu Naibu aesema Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2021 ndiyo ulionyesha tatizo hilo ndani ya nchi jambo ambalo limewekewa mkakati katika kuhakikisha vijana wanaandaliwa ili waweze kushindana katika soko la ajira.
“Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ujuzi wa Miaka 10 (2016/2017 – 2025/2026) ambapo Kupitia Mkakati huu, Serikali imefanya maboresho ya miundombinu na mitaala katika ngazi za Elimu ya Juu, Elimu ya Kati, na Mafunzo ya Ufundi Stadi,” amesema Katambi.
Amesema sambamba na maboresho hayo, Serikali inatoa mafunzo ya kuwezesha vijana walio nje ya mfumo rasmi wa mafunzo ili kumudu ushindani katika katika soko la ajira yakiwemo mafunzo ya uanagenzi.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo mafunzo mengine ni uzoefu wa kazi (internship) kwa wahitimu; mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo (RPL.