Wanafunzi 11,413 ambao ni asilimia 45 ya wanafunzi 25,362 waliotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule wa sekondari mkoani hapa hawajaripoti shuleni tangu shule hizo zilipofunguliwa Januari 9 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga amesema hayo Februari 2, 2023 wakati akitoa maelekezo kwa wakuu wapya wa wilaya katika wilaya za Sumbawanga na Kalambo.
Wakuu hao wa wilaya walioapishwa ni Dk Jane Nyamsenda ambaye atahudumu Wilaya ya Sumbawanga na Lazaro Komba aliyeenda Wilaya ya Kalambo.
Kufuatia kundi kubwa la wanafunzi kutokuripoti shuleni ameagiza kufanyika kwa masako wa nyumba hadi nyumba ili kuwabaini watoto ambao hawajaripoti shuleni ili waanze kwenda shule haraka iwezekanavyo.
Aidha, amewataka wakuu hao wa wilaya kushughulikia changamoto ya ukosefu wa madawati katika shule za msingi ambapo wanafunzi wanakaa sakafuni kutokana na kukosekana kwa madawati 13,458.
“Nindeni mkashughulikie changamoto ya madawati ambapo wilaya ya Kalambo tunahitaji madawati 1,209, Sumbawanga 4,649 na Nkasi ni 7,600 ifikapo Februari 28 sitaki kusikia wala kuona watoto wanakaa chini,” amesema.
Pia amewataka kusimamia miradi ya maendeleo, ikiwemo kuhakikisha miradi yote iliyoibuliwa wananchi ikiwemo zanahati na vituo vya afya inakamilika.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Jane Nyamsande amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wake huku akiahidi kufanya kazi kwa weledi na maarifa ili kufanikisha lengo la Serikali kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Silafu Maufi amewataka wateule hao wa Rais kufanya kazi kwa ushirikiano ili waweze kuwaletea wananchi maendeleo kwenye maeneo wanayokwenda kuyaoongoza.