Afisa wa polisi amekamatwa kwa kupoteza bunduki yake mjini Kendu Bay, Rachuonyo kaunti ya Homa Bay.
Afisa huyo aliyetambulika kwa jina Koplo Micah Chesang anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Kendu Bay, alibambwa baada ya bastola aina ya Ceska aliyokabidhiwa kupotea katika hali isiyoeleweka.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika Kaunti ya Homa Bay Abed Kavoo, alithibitisha kuwa afisa huyo wa polisi alikamatwa na anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay.
“Afisa huyo anatusaidia katika uchunguzi kwa sababu tunahitaji ukweli zaidi kuhusiana na suala hilo katika azma yetu ya kuhakikisha haiko katika mikono hatari,” alisema Kavoo.
Inaripotiwa kuwa afisa huyo wa polisi alipewa bunduki hiyo siku ya Jumamosi, Februari 4, kushika doroa usiki katika eneo la Kendu Bay.
Afisa huyo alitekeleza jukumu hilo kwa mafanikio hadi aliporejea katika nyumba yake ya kupangisha iliyoko kaunti ndogo ya Konyango Kaskazini, Mashariki mwa eneo la Karachuonyo mwendo wa saa 10 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, afisa huyo alikwenda kulala na kuiweka bunduki hiyo chini ya mto.
Aliamka saa kumi asubuhi kwenda kujisaidia na wakati aliporejea, alikuta bunduki hiyo haipo.
Kisha afisa huyo alipiga ripoti kuhusu kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Kendu Bay mnamo Jumapili, Februari 5, asubuhi.
Baada ya kupiga ripoti, maafisa wenzake walipekua nyumba yake kuitafuta silaha hiyo lakini hawakuipata na hivyo kusababisha kukamatwa kwa afisa huyo.
Kulingana na Kavoo, maelezo ya afisa huyo yalikuwa na shaka na hivyo kusababisha kukamatwa kwake. “Ofisa anayehusika ana wiki mbili tu kituoni hapo, na majirani zake walisema madirisha ya nyumba zao yamevunjwa.
Hizi ndizo kauli tunazotumia kutafuta ukweli ambao unaweza kufichwa,” alibainisha.