Mbunge wa Lang’ata Felix Odiwuor amesema siasa ni karata ambayo inahitaji ujanja wa sungura ili mtu kudumu.
Akitetea hatua yake ya kufika Ikulu kukutana na Rais William Ruto licha ya kuwa mbunge wa ODM, Jalang’o amesema wakati wa siasa uliishi na sasa ni kipindi cha kufanyia wananchi kazi.
“Watu wa Lang’ata hawataki kujua ni nani yuko Ikulu. Wanachotaka ni wafanyiwe kazi ile ambayo walinipa,” alisema Jalang’o.
Jalang’o alichaguliwa kwa tiketi ya ODM baada ya kuungwa mkono na Raila Odinga ambaye kwa sasa anampinga Rais Ruto.
Raila amekuwa akifanya mikutano ya kisiasa ksuhinikiza Rais Ruto kujiuzulu akisema aliiba kura kwenye uchaguzi wa urais.
Jalang’o amekuwa mmoja wa wale ambao huhudhuria mikutano ya Raila lakini sasa anaonekana kuchukua mkondo mpya.
“Hata kama Raila angeniambia nisihudhurie mkutano wa Rais Ruto katika Ikulu bado ningefika huko,” alisema mbunge huyo anayehudumu kipindi cha kwanza.
Kwa mujibu wake, mikutano ya Raila haina umuhimu wowote kwake na kwa wakazi wa Lang’ata iwapo masuala ya maendeleo hayatashughulikiwa.
“Hata nikienda mkutano wa Raila na Lang’atra hakuna maji, hakuna atakayejali eti nilikuwa mkutano. Lakini wakiwa na maji na hata nikose kuhudhuria mkutano watakuwa sawa,” aliongeza mbunge huyo.
Ziara ya Jalang’o na wenzake ikulu ambapo walikutana na uongozi wa Kenya Kwanza imezua joto kali la kisiasa ndani ya chama cha ODM.
Wenzao kwenye ODM waliwapuuza wakisema walikuwa wamefika Ikulu kujitafutia vyao na wala si kwa maslahi ya wananchi.