Katika hali ya kusikitisha mzee wa miaka 80 mkazi wa Kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga, Luhende Tungwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka mjukuu wake anayesoma Shule ya Msingi Old Shinyanga (jina limehifadhiwa) baada ya kutoka shule.
Tukio hilo limetokea jana mchana baada ya mwanafunzi huyo kutoka shule na kumkuta babu yake, huku bibi akiwa ameenda shambani, ndipo mtuhumiwa aliamua kutumia fursa hiyo kufanya kitendo hicho dhidi ya mjukuu wake.
Kwa upande wake, bibi wa mjukuu aliyefanyiwa ukatili huo, Mariam Kishiwa mkazi wa Kijiji cha Ihapa amesema alikuwa shambani na baada ya kurudi na kumuona mtoto anaumwa, alimhoji na kumjibu kwamba alipoamechomwa na mti sehemu za siri.
Hata hivyo baada ya kumwangalia alikuta anatiririka damu, alichukua jukumu la kumpeleka shuleni alimkuta mwalimu mkuu na kumwambia kuwa mtoto ameumia.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Old Shinyanga, Judith Julias baada ya kumwangalia alibaini mtoto huyo amebakwa, ndipo wakampeleka mwanafunzi huyo Zahanati ya Old Shinyanga, lakini walipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga, pia mwalimu alitoa taarifa kwa afisa maendeleo diwani na afisa elimu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo amesema baada ya kuona mtoto kuwa na viashiria vya kubakwa, alimdadisi na mtoto huyo alisema kuwa amemefanyiwa kitendo hicho na babu yake baada ya kutoka shule nà kumkuta babu akiwa peke yake nyumbani.
“Alipokuja hapa bibi wa mtoto na mtoto aliniambia amefanyiwa kitendo hicho wakati akitoka shule lakini baada ya kumhoji vizuri kuwa nani aliyemfanyia kitendo hicho alimtaja babu yake, katika shule yetu tunafanya jitihada za kuwalinda watoto pindi wakiwa shuleni na pindi wanapoondoka, kwa kweli kitendo hiki ni cha unyama hivyo tuwaombe jamii iwalinde watoto,” amesema mwalimu Julius.
Dk Jusitina Tizeba bingwa wa magonjwa ya watoto katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga amesema wamempokea mtoto akiwa na hali mbaya wamempatia matibabu anaendelea vizuri na maumivu yamepungua.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amesema vitendo hivyo vinatokana na kuporomoka kwa maadili kwenye jamii,hivyo aliiomba jamii iache kufanya vitendo kama hivyo iwe na hofu ya Mungu.
Diwani Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga, Pica Chogelo alipata taarifa kutoka kwa mwalimu mkuu kwamba mtoto amefanyiwa ukatili wa kubakwa, baada ya kufika kwa mtoto huyo walikuta hali sio nzuri ambapo alianza na kutapika.
“Kutokana na matukio haya kuendelea kutokea ninaiomba serikali iendelee kutoa elimu na kwa yeyote anayefanya vitendo kama hivi achukuliwe hatua kali za kisheria ili iweze kuwa fundisho kwa jamii,” amesema Chogelo.
Afisa Maendeleo Kata ya Old Shinyanga, Enea Boniface baada ya kupata taarifa wamekwenda na kumkuta mtoto ameumizwa, hivyo ameiomba jamii kukemea tabia hiyo na kukomesha kabisa ukatili dhidi ya watoto.