Kanisa la Anglikana (ACT) limemchagua kwa mara ya nyingine Askofu wa Dayosisi ya Tanga, Maimbo Mndolwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo.
Katika uchaguzi wenye ushindani mkali uliofanyika Februa 9, 2023, Askofu Mndolwa alimshinda Askofu Dk Stanley Hotay wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
Katibu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Tanzania, Mchungaji Canon Bethuel Mlula amesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkali maaskofu wenye umri wa chini ya miaka 60 wote walikuwa wanapigiwa kura.
“Kura zingine hatuwezi kuzitaja maana kuna wengine walikuwa wanapata kura moja, mbili au tatu hivyo nakutajia majina matatu ambayo yalikuwa kwenye ushindani mkali,” alisema Mchungaji Mlula.
Maaskofu hao walichuana tangu awamu ya kwanza ambapo Mndolwa alipata kura 55 huku Dk Hotay akipata kura 52.
Awamu ya pili bado wawili hao walitofautiana kwa kura tatu tena baada ya Mndolwa kuibuka na kura 65 na Hotay akipata kura 62 na wakati wote Askofu James Almas wa Dayosisi ya Masasi alikuwa akipata kura 11.
Katika awamu ya mwisho ambapo yalibaki majina mawili, Askofu Mndolwa aliyekuwa akitetea nafasi hiyo alipata kura 77 na mshindani wake akapata kura 61 hivyo kuamua ushindi wa jumla kwa Mndolwa.