KUFUATIA kuzagaa kwa tetesi kuwa kuna timu kutoka barani Ulaya zimeonyesha nia ya kumsajili straika wa Simba, Jean Baleke, uongozi wa Simba kupitia kwa Meneja wake wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally umechimba mkwara mzito kuwa hakuna mchezaji yeyote wa timu hiyo aliye kwenye mipango yao ambaye ataondoka.
Baleke ambaye anakipiga Simba kwa mkataba wa mkopo wa miaka miwili akitokea TP Mazembe ya DR Congo, mpaka sasa amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja na nusu kuhudumu ndani ya Simba huku kukiwa na kipengele cha kuweza kumuongezea mkataba.
Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo ambaye alijiunga na Simba katika kipindi cha dirisha dogo la usajili, amekuwa na wakati mzuri ndani ya kikosi hicho akifunga zaidi ya mabao 13 kwenye mashindano yote kwenye kipindi cha muda mfupi kiasi cha kuzitamanisha timu kubwa kuhitaji saini yake.
Akizungumzia tetesi hizo, Ahmed alisema: “Ni jambo lililo wazi kuwa unapokuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa unapaswa kutegemea tetesi nyingi kipindi cha usajili kama vile Mohammed Hussein anatakiwa na timu za Afrika Kusini, Manula kutajwa Azam au Baleke kutakiwa na timu za Ulaya.
“Lakini niwathibitishie Wanasimba kuwa hakuna mchezaji ambae yupo kwenye mipango yetu ataondoka, Wale waliomaliza mkataba na tunawahitaji watasalia kwenye maboresho tunayoyafanya ni pamoja na kuwabakisha wale tunaowahitaji.”