Mshambuliaji wa Argentina na Paris St-Germainm, Lionel Messi amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa wanaume kwenye Tuzo za Fifa za 2022.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 aliwashinda washambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe na Karim Benzema.
Messi aliwahi kuwa nahodha wa Argentina na kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Qatar, na alifunga mabao 27 katika michezo 49 kwa klabu na nchi yake mnamo 2021-22.
Alexia Putellas wa Barcelona alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa wanawake.
Messi, ambaye alishinda tuzo hiyo kwa mara ya pili, alisema: “Inashangaza. Umekuwa mwaka mzuri sana na ni heshima kwangu kuwa hapa na kushinda tuzo hii. Bila wachezaji wenzangu nisingekuwa hapa. “Nilifanikisha ndoto niliyokuwa nikitarajia kwa muda mrefu. Watu wachache sana wanaweza kufikia hilo na nimekuwa na bahati kufanya hivyo.”
Katika sherehe hizo mjini Paris, Lionel Scaloni, ambaye aliiongoza Argentina kutwaa taji lao la tatu la Kombe la Dunia, alitawazwa kuwa kocha bora wa mwaka wa wanaume.
Scaloni aliwashinda Pep Guardiola ambaye aliiongoza Manchester City kunyakua taji la sita la Ligi ya Premia na mkufunzi wa Real Madrid aliyeshinda Ligi ya Mabingwa, Carlo Ancelotti kwa heshima.
Kocha wa England, Sarina Wiegman alitawazwa kuwa kocha bora wa mwaka wa wanawake baada ya kukiongoza kikosi cha England kutwaa ubingwa wa Ulaya katika ardhi ya nyumbani mwaka jana, likiwa ni taji la kwanza kuu kwa timu hiyo.
Mlinda mlango wa Aston Villa na Argentina Emiliano Martinez alitambuliwa kuwa mlinda mlango bora wa wanaume, huku Muingereza Mary Earps akishinda tuzo ya wanawake.
Martinez, 30, aliisaidia nchi yake kushinda Kombe la Dunia, akiokoa penalti nne ikiwa ni pamoja na ushindi wa mikwaju dhidi ya Ufaransa kwenye fainali.
Earps, anayechezea Manchester United katika Ligi Kuu ya Wanawake, alianza mechi zote sita za England kwenye Euro 2022 huku wakishinda michuano hiyo.