KIUNGO mshambuliaji wa Simba Mzambia, Clatous Chama amewaomba msamaha mashabiki wa timu hiyo, baada ya kukosa mataji katika msimu huu huku akiwaambia kuwa mengi yanakuja msimu ujao.
Simba ilianza kwa kupoteza Kombe la FA baada ya kutolewa dhidi ya Azam FC katika mchezo wa nusu fainali ya mashindano kwa kufungwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Timu hiyo, juzi ilipoteza rasmi ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya Yanga kutangazwa mabingwa wa taji hilo kwa kuwafunga Dodoma Jiji mabao 4-2.
Akizungumza Mei 15, Chama alisema kuwa wao wachezaji wamechukizwa kukosa kombe lolote katika msimu huu huku wakijipanga vizuri kuhakikisha wanabeba mataji yote ya ndani katika msimu ujao.
Chama alisema kitu kingine walichokipanga ambacho lazima wakitimize ni kufuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu ujao, baada ya kuishia robo fainali katika misimu minne tofauti.
Aliongeza kuwa zipo sababu nyingi zilizosababisha wao wapoteze yote katika msimu huu, lakini uzuri kwamba viongozi na benchi la ufundi lililo chini ya Mbrazili, Robert Oliviera ‘Robertinho’ wanafahamu walipokosea hivyo watarejea kivingine msimu ujao.
“Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea kukosa ubingwa timu yoyote ikakosa ubingwa kama ilivyokuwa kwetu, wakati mwingine sababu zinaweza kuwa nje au ndani ya uwanja.
“Tuwaambie mashabiki wa Simba kuwa tutarejea msimu mwingine na zaidi kupambania ubingwa wa ligi na Kombe la FA, tunafahamu tulipokosea tutarejea tukiwa kamili kufanikisha malengo yetu.
“Hakuna kitakachoshindikana kwetu, zaidi ya sisi wachezaji wenyewe kufahamu sababu iliyosababisha kukosa makombe msimu huu,” alisema Chama.