Ametoa rai hiyo wakati akitoa neno la utangulizi katika mkutano wa 16 wa Baraza la Kisekta la Kilimo na Usalama wa Chakula la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia kilimo, chakula, uvuvi na ukuzaji viumbe maji hii leo Mei 19, 2023 Dar es Salaam.
Amesema uwekezaji ukiongezeka utachechemua uzalishaji na hivyo kuimarisha usalama wa chakula na pia kutashamirisha biashara ya chakula miongoni mwa nchi hizo na kukuza uchumi wao.
Aidha Waziri Ulega amesema kwa upande wa serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kufanya uwekezaji kwenye sekta za mifugo na uvuvi na kilimo ziweze kuongeza uzalishaji ili ziwe na mchango mkubwa zaidi katika pato la Taifa.
Miongoni mwa hatua alizozitaja ambazo Dkt. Samia Suluhu Hassan amezichukua ni pamoja na kuwawezesha vijana mitaji ya kujiajiri kupitia sekta za mifugo, uvuvi na kilimo, kuwawezesha maafisa ugani ili watoe huduma sahihi na kwa urahisi kwa wananchi, Kutekeleza Mpango Kabambe wa sekta ya Uvuvi wa Mwaka 2021/2022- 2036/2037 na kufanya kampeni kubwa ya uchanjaji na uogeshaji wa mifugo nchini.
Mkutano huo ulikutanisha Mawaziri 7 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.