Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ameagiza wanufaika wa fidia waliopisha miradi ya Liganga na Mchuchuma kuambatana na familia zao siku ya ulipwaji wa fedha ili familia zijue na kuepusha udanganyifu unaoweza kufanywa na wanufaika.
Mtaka amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea June 7 siku ambayo Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji kwa niaba ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan atashuhudia uzinduzi wa zoezi la ulipwaji wa fedha kwa wanufaika 1142 katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa.
“Tumewaalika wanufaika wote na familia zao kwasababu tumeona mifano mingi unakuta mtu anlipwa hela kwenye account halafu anakaa nyumbani anasema serikali inajenga miradi mikubwa lakini haijamlipa fidia,na mtoto wake akija kwenye mitandao anaanza kutukana serikali kumbe baba yake alishalipwa hela mwaka mmoja uliopita”amesema Mtaka
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Maendeleo la Taifa NDC Dkt.Nicolaus Shombe amesema kiasi cha shilingi Bilioni 15.4 kinakwenda kulipwa baada ya hadithi za takribani miaka 40 ambapo zoezi hilo linakwenda kufanywa kwa uwazi ili kuepuka migogoro kwa wananchi na kuilamu serikali kuwa imeshindwa kulipa stahiki zao.