Na Evelyne Ernest
HOFU na huzuni vimewagubika wananchi wa mtaa wa Omukituri, uliopo kata ya Kibeta, manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, baada ya Conchester Gervazi, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 32 ambaye ni Mke wa Mwenyekiti wa Mtaa huo, kukutwa ameuawa asubuhi ya Juni 13, mwaka huu, huku chanzo cha kifo hicho kikiwa bado hakijajulikana.
Akizungumza na Waandishi wa habari kutoka eneo la tukio, Anajoyce Deus, ambaye ni Mama mkwe wa marehemu, amesema usiku wa saa tatu ya Juni 12, mwaka huu, alikutana na Conchester katika eneo la nyumba ya jirani kisha kuagana naye lakini cha kushangaza asubuhi ya Juni 13, majira ya saa 12 za asubuhi, alisikia sauti yenye kelele iliyopigwa na mtoto wake, hivyo kutoka nje na kuelezwa kuwa mkwe wake amelala chini huku akipandwa na wadudu kisha kuanza kuwaita majirani ili waweze kufika na kushuhudia tukio hilo la kinyama, huku akiongeza kuwa hakuwa na mgogoro wowote na marehemu kwani walikuwa wanapendana sana.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Gypson Godson, akizungumza kwa masikitiko makubwa kufuatia tukio hilo, amesema marehemu ameuawa karibu na nyumbani kwake na mwili wake umeonekana kupigwa na kifaa butu karibu na eneo la shingo, huku akiwasihi wananchi kuendelea kuwa watulivu hadi pale Jeshi la Polisi litakapokamilisha kazi yake ya upelelezi na taarifa rasmi kutolewa na vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Naye diwani wa kata ya Kibeta, Anastela Alphonce, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, amemtaja mwenyekiti wa mtaa huo kuwa ni Gervazi Nyomo, na kwamba kabla ya tukio hilo wanandoa hao walikuwa wakiishi vyema pasipo na vurugu, na kuongeza kuwa taarifa ya unyama huo amezipata asubuhi ya Juni 13, ambapo alifika na kuwakuta maafisa wa Jeshi la Polisi wakiendelea na uchunguzi huku baadhi ya wanafamilia wakiangua vilio kwa uchungu.