JKT Tanzania imeendelea kujiimarisha ili kutisha kwenye Ligi Kuu msimu ujao baada ya kupanda msimu huu ikitokea Championship ilikokuwa mabingwa na sasa imenasa saini ya beki wa kulia, George Aman Wawa kutoka Geita Gold ikimpa mkataba wa miaka miwili.
Wawa amekuwa mchezaji wa tatu kwa JKT kumchomoa Geita katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu baada ya hapo awali kuwanasa Danny Lyanga na Deusdedith Okoyo kwa ajili ya msimu ujao.
JKT imempata Wawa akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na matajiri hao wa Geita.
Sambamba na Wawa, Okoyo na Lyanga, JKT Pia imekwisha nasa saini ya Ismail Aziz Kader aliyetemwa na Azam na iko mbioni kukamilisha usajili wa kiungo wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Said Ndemla.
Akizungumza kocha mkuu wa JKT Tanzania alifunguka lazima aongeze wachezaji wapya kwenye kikosi chake ili kuendana na kasi ya Ligi Kuu.
“Tutafanya usajili mkubwa. Ujue Championship ni tofauti na Ligi Kuu, hivyo lazima tuwe na wachezaji wanaoweza kuendana na kasi ya ligi hiyo kwa msimu ujao,” alisema Malale aliyeipandisha JKT daraja.