Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kuwashikilia na kuwahoji viongozi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wapatao 520 na kuwaachia huru baadhi yao kwa dhamana.
Aidha Jeshi la Polisi limesema wale ambao hawakuachiwa ni wale walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana au kuwa na makosa zaidi ya moja, ikiwemo jinai huku likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.
Akizungumza usiku wa kuamkia Agosti 13, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo nchini, Awadhi Haji amesema Agosti 11 walikamatwa 375, ikiwa wanaume 261 na wanawake 114 na Agosti 12 wamekamata 145, wanaume 112 na wanawake 33.
“Kati ya watuhumiwa waliokamatwa kwa kosa la kukaidi kuendelea na safari kuja Mbeya, walikuwemo viongozi wakuu wa Chadema waliokamatiwa mkoani hapa eneo la Kadege, ambao ni Makamu Mwenyekiti Tundu Lisu, Katibu Mkuu, John Mnyika, Mwenyekiti wa Kanda, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Katibu Mwenezi wa Bavicha Taifa, Twaha Mwaipaya na Makamu Bavicha, Moza Ally.
Mnamo Agosti 12 Jeshi la Polisi liliwakamata wafuasi wengine 145 wakiwamo viongozi wakuu wa chama hicho Taifa, ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mwenyekiti Bavicha Taifa, John Pambalu katika Uwanja wa Ndege Songwe wakija kushiriki kongamano lililopigwa marufuku na kufanya jumla ya waliokamatwa kufikia 520” amesema Kamanda Haji.
Kamanda huyo amesema kuwa watuhumiwa wote walihojiwa kisha kurejeshwa maeneo walipotoka kwa kusindikizwa na Polisi huku waliokamatwa kutoka Mkoa wa Mbeya wakipewa dhamana.