Katika hali ya kushangaza ndugu wawili (Kaka na Dada) wote wamezaliwa Baba na Mama mmoja, wamefungwa jela mmoja miaka 20 na mwingine miaka 30 kwa kosa la kuoana, kuzini na kuishi kama mke na mme takribani miaka 7 wakijua kabisa kuwa ni ndugu wa damu.
Hukumu hiyo imetolewa jana Agusti 14, 2024 na Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, ambapo Kesi hiyo jinai namba 26634/2024 ilikuwa chini ya Hakimu mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo Enos Misana.
Ndugu hao walihukumiwa kifungo hicho ni Mussa Shija (33) ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 20 na Hollo Shija (35) aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela wote wakazi wa Kijiji Cha Mandang’ombe Wilayani Maswa Mkoani Simiyu.
Kabla ya hukumu kutolewa, akisoma kosa lao Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka ya Taifa wilaya ya Maswa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Vedastus Wajanga kuwa walitenda makosa hayo tarehe na miezi tofauti kati mwaka 2018 hadi tarehe 31/07/2024 katika kijiji cha Mandang’ombe wilayani humo.
Wajanga alielezea Mahakama kuwa Washtakiwa hao ni ndugu wa damu (kaka na dada) na wanazaliwa na Baba na Mama mmoja na katika mahusiano yao walikuwa wakiishi kama mke na Mme na wamebahatika kupata mtoto mmoja mwaka 2022.
Mwendesha Mashtaka huyo aliendelea kuelezea Mahakama kuwa Makosa waliotenda ni Mwanaume kujamiana na Maharimu (Kufanya ngono na ndugu yako wa damu) kinyume na kifungu cha158 (1) (b) na Mwanamke kujamiana na maharimu kinyume na kifungu 160 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.
Baada ya kusomewa Mashitaka yao, mbele ya Hakimu huyo washtakiwa hao walikiri hapo hapo huku wakijitetea kuwa kitendo walichokifanya wao walikuwa hawajui kuwa ni kosa kwani walishawishiwa na Babu yao mzaa baba kwa lengo la kudumisha mila za ukoo wao kwa kutakiwa kuoana.
Mara baada yakukiri makosa yao Mahakama hiyo iliwatia hatiani na Hakimu kumhukumu mshtakiwa wa kwanza Mussa Shija kwenda jela miaka 20 na mshtakiwa wa pili Hollo Shija kwenda jela miaka 30.