Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Hamza Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Johari ambaye kabla ya uteuzi huu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) anachukua nafasi ya Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Rais Samia pia amemteua Samwel Maneno kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kabla ya uteuzi huu, Maneno alikuwa Msaidizi wa Rais, Sheria na anachukua nafasi ya Balozi Prof. Kennedy Gastorn ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Sheria na Mikataba.
Vilevile Rais Samia amemteua Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Wakili Mkuu wa Serikali, kabla ya uteuzi huu, Dkt. Possi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi.