Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la mto Hurui lililopo kata ya Kikore Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma huku akiwahimiza wananchi wa kata ya Kikore na watumiaji wa daraja hilo kutunza miundombinu iliyojengwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
Aidha ametumia nafasi hiyo amewameiagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kufanya ukarabati wa Barabara ya Ntundwa – Hurui ya Wilayani Kondoa ili kuwarahisishisa wananchi shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji mazao.
Maagizo hayo ameyatoa jana jijini hapa mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la mto Hurui lililopo kata ya Kikore Wilayani Kondoa ambapo ameagiza kupandwa miti maeneo yote ya pemebezoni mwa mto hurui ili kuokoa daraja hilo lisiharibike kutokana na mmomonyoko wa udongo.
Mbali na hayo aliwapongeza wananchi hao kwa kupata mradi wa daraja hilo ambalo litawaondolea changamoto waliyopata ya kukosa daraja tangu mwaka 2019 lilipoharibiwa na maji daraja la awali.
Sambamba na hayo amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itaendelea kuwafikishia wananchi huduma muhimu ikiwemo miundombinu ya umeme.
Akiwa kata ya Kikore ameagiza kukamilishwa kwa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata hiyo ifikapo tarehe 30 mwezi Oktoba 2024.
“Naiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini kushughulikia changamoto iliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Hurui kuhusu ardhi ya Kijiji inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji bila kufuata utaratibu, “alisema
Ujenzi wa Daraja la Hurui umegharimu shilingi bilioni 1.6 na linatarajiwa kuwa kiungo muhimu na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa kurejesha mawasiliano kati ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Daraja hilo lenye urefu wa Mita 30 limejengwa kwenye barabara ya Ntundwa – Mkunduru -Hurui yenye urefu wa kilometa 46.4. Mradi huo umehusisha uboreshaji wa kilometa 8 za barabara kwa kiwango cha changarawe na umegharamiwa na Serikali kupitia tozo ya mafuta ya shilingi 100.