Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio, jana alishinda kwa kishindo nafasi na Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni baada ya kujizolea kura zote 21 zilizopigwa kwenye uchaguzi wa kugombea kiti hicho.
Akimtangaza kushinda nafasi kiti hicho, Meya wa Manispaa hiyo, Songoro Mnyonge amempongeza kwa ushindi huo na kumuahidi kushirikiana naye vyema kwenye majukumu yake mapya aliyoanza kuyatekeleza hapo jana.
Baada ya kutangazwa ushindi huo Ukumbi wa Baraza la Madiwani hao ulipofanyika uchaguzi huo ulilipuka kwa mayowe ya vifijo na nderemo za kumshangilia kiongozi anayeaminika kuja kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwenye Manispaa hiyo.
Imani ya mabadiliko hayo inafuatia mambo makubwa aliyoyafanya kwenye Kata ya Kunduchi katika kuboresha huduma za afya, elimu, makazi, miundombinu na mengineyo.
Kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya kwenye kata hiyo wakazi wa kaya yake wameamua kuipa jina lake moja ya shule za kata hiyo ambapo shule hiyo inaitwa Michael Urio Sekondari. Alisema mmoja wa wakazi wa Kata hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Salma Kada.
Akizungumza machache baada ya kushinda nafasi hiyo, Naibu Meya Urio aliwashukuru madiwani wenzake waliomuamini na kumpa ushindi huo wa kishindo na kuwaahidi kushirikiana nao pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Meya wake Songoro Mnyonge na viongozi wengine katika kusongesha vyema maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada tu ya kumaliza shughuli za kumtangaza Naibu Meya Urio kwake ilikuwa hakuna kupumzika aliingia kwenye ofisi yake mpya na kuanza kuikagua kwa ajili ya kuanza kupiga kazi.
Miongoni mwa waliofika kushuhudia uchaguzi huo ni wageni kutoka sehemu mbalimbali pamoja na viongozi wa kidini wakiwemo mashehe na wachungaji akiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa la Mungu Baba Halisi aitwae Baba Halisi lenye Makao yake Makuu, Tegeta jijini Dar.