Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga Mhe. Joseph Modest Mkude ameagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kishapu kuhakikisha inakamilisha miradi ya maji ifikapo Desemba 2024 ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mhe. Mkude ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Agosti 23,2024 wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Maji Wilaya ya Kishapu ulioandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wenye lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Maji na Usafi wa Mazingira.
“Kwenye yale maeneo ambayo miradi bado haijakamilika, naagiza hadi Mwezi Desemba 2024 miradi ambayo fedha zake zimekuja iwe imekamilika ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama”,amesema Mhe. Mkude.
Mhe. Mkude ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji hivyo kuwaomba wananchi kutunza miradi ya maji ili iwe endelevu.
Aidha amewaomba wadau wa maji kuendelea kushirikiana na serikali kutoa huduma za maji safi na salama huku akiwataka wataalamu kuendelea kutoa mwongozo kwa wananchi kuhusu uchimbaji wa visima ili kuifanya Kishapu kuwa na vyanzo vingi vya maji.
“Maeneo ambayo tayari huduma ya maji imefika lakini kuna changamoto ya madeni ya Ankara inaturudisha nyuma kwenye maendeleo ya miradi. Madeni yaliyopo kwenye taasisi zinazodaiwa wahusika wawajibike”,amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson ameagiza Taasisi zinazodaiwa zishughulikiwe kama taasisi zingine huku akiagiza RUWASA kukata huduma ya maji kwenye taasisi hizo kwani zina wajibu wa kulipa Ankara za maji.
“Kama kuna taasisi ya serikali ipo kwenye halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inadaiwa ilipe deni, natoa muda wa mwezi mmoja kama zinadaiwa Ankara ya maji zilipe, kama kuna taasisi itakuwa haijalipa mimi nitachukua hatua, ”,amesema Johnson.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Dickson Kamazima amesema kipaumbele ni kuyafikia maeneo ambayo hayana huduma akibainisha kuwa wadau wa maji wanalo jukumu la kuendelea kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya maji safi na salama ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji na miundombinu ya miradi ya maji kwani kumekuwa na uharibifu mkubwa kwenye miradi.
Amesema pia wadau wana wajibu wa kulipa Ankara za maji kwa ajili ya gharama za uendeshaji na matengenezo ya skimu hususani taasisi za serikali kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya.
Hata hivyo amesema wapo baadhi ya viongozi wanaishawishi jamii kutotumia maji ya visima ili waweze kuletewa maji ya Ziwa Victoria na kubainisha kuwa wakati zoezi la kusambaza maji ya Ziwa Victoria kupitia bomba la KASHWASA lakini pia RUWASA inaendelea kusambaza maji kwa wananchi kwa kutumia vyanzo vingine vya maji kama vile visima virefu, visima vifupi,mabwawa na mito.
“Kila mmoja wetu atambue kuwa yeye ni mdau muhimu katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana na inakuwa endelevu, tunatambua bado kuna vijiji zaidi ya 40 ambavyo havina huduma ya maji safi na salama, lakini tunayo mipango katika maeneo hayo na kadri tunavyopata fedha, tunaendelea kujenga miradi na kupanua miradi ili kuwafikia wananchi wengi zaidi”,ameeleza Mhandisi Kamazima.
“Tunaendelea kuwakaribisha wadau wa maendeleo wa sekta ya maji zikiwemo NGO’s tushirikiane katika ujenzi wa miradi kwenye maeneo ambayo bado hayana huduma ya maji. Mwingine anaweza kujenga chanzo cha maji, mwingine akajenga miundombinu ya matangi na mwingine akajenga miundombinu ya usambazaji maji na siyo lazima mradi mzima ajenge mtu mmoja bali tushirikianena maeneo mengine wanafanya hivyo, lengo ni kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wetu”,ameongeza Mhandisi Kamazima.
Amesema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni baadhi ya taasisi za umma kutolipa Ankara za maji kwa wakati na zingine hazilipi kabisa hali inayochangia huduma za maji kutotolewa ambapo kutokana na ulipaji hafifu wa madeni kwa taasisi wanadai zaidi ya shilingi Milioni 13.