Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma imepanga kutoa hati ya ukamatwaji wa mtu anayetambulika kama Afande, Fatmah Kigondo anayedaiwa kuratibu tukio la ubakwaji na ulawiti wa binti wa Yombo Dar es Salaam endapo kama hatofika mahakamani.
Hatua hiyo inakuja baada ya mlalamikaji ambaye pia ni Wakili Paul Kisabo kumfungulia kesi namba 23627 ya mwaka 2024 Afande Kigondo ambapo kesi hiyo ilianza kusikilizwa kuanzia saa 6:30 mchana hadi saa 6:52 mchana mbele ya Hakimu Francis Kishenyi.
Hata hiyo imeelezwa mahakamani hapo kwamba licha ya mlalamikiwa kupewa wito ambao unasemekana umemfikia lakini hakufika mahakamani hapo.
Nje ya viunga vya mahakam tumezungumza na Wakili wa mlalamikaji ambaye ni Peter Madeleka;
“Moja kati ya jambo ambalo limejadiliwa ni kwanini mlalamikiwa hajafika mahakamani, ikizingatiwa ukweli kwamba hati ya kuitwa mahakamani imetolewa jana tarehe 22/8/2024 na sisi tukaipata ni wazi kwamba mlalamikiwa hajafika mahakamani, hivyo tumeiomba mahakama itoe hati ya ukamatwaji kwamba akamatwe kwa sababu kwanza hii ni kesi ya jinai kwamba mshtakiwa ama mlalamikiwa anatakiwa afikishwe mahakamani akiwa chini ya ulinzi kwa sababu malalamiko haya yameletwa na mtu ambaye hana mamlaka hayo ili yaweze kutimizwa matakwa ya kisheria mahakama itoe hati ya ukamatwaji kwa sababu mlalamikiwa hajafika mahakamani bila sababu za msingi, hivyo baada ya mahakama kujadili hoja hiyo imekubali kwamba ni kweli wito ulitolewa jana na bahati mbaya ama nzuri kwa sababu anazozijua afande hajafika mahakamani, hivyo imeomba na kutoa amri kwamba hati ya ukamataji itatolewa Septemba 5, 2024 ikiwa Afande hatofika mahakamani na kukaidi amri ya mahakama,”