Msako mkubwa umeanzishwa baada ya watu watatu kuuawa na wengine nane kujeruhiwa katika shambulio la kisu katika mji wa magharibi wa Ujerumani wa Solingen, polisi wamesema.
Shambulio hilo lilitokea katika tamasha lililokuwa likifanyika katikati mwa mji huo Ijumaa jioni. Watano kati ya watu nane waliojeruhiwa wako katika hali mbaya, kwa mujibu wa vyombo ya habari vya Ujerumani.
Polisi Jumamosi walisema kwamba bado wanamsaka mshambuliaji huyo, lakini hawakutoa maelezo kuhusu nia ya kutekeleza kitendo hicho.
Mtu huyo anaripotiwa kuwashambulia wapita njia kwa kisu wakati waakazi walipokuwa wakisherehekea miaka 650 tangu kuanzishwa kwa mji huo.
Inaaminika kuwa mtu huyo alilenga kuwadunga watu hao kwenye shingo, kwa mujibu wa taarifa za habari nchini humo.
Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema Jumamosi kuwa mtu huyo lazima akamatwe haraka na kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.