Mgombea wa kujitegemea katika uchaguzi wa urais Marekani Robert F Kennedy Jr ameungana na mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, jukwaani katika mkutano wa kampeni huko Arizona baada ya kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono rais huyo wa zamani wa Marekani.
Kennedy, mwenye umri wa miaka 70, aliyekuwa mwanachama wa Democrats kwa kipindi kirefu katika maisha yake na anayetokea kwenye familia kubwa ya Kennedy, alisema kwamba maadili yaliyomfanya aondoke kwenye chama hicho sasa yamemshawishi “kujitosa nyuma ya rais Trump na kumuunga mkono”.
Katika kikao na waandishi wa habari huko Phoenix, Arizona, siku ya Ijumaa, Kennedy alisema kwamba angeanza mchakato wa kuondoa jina lake kwenye karatasi za kura katika majimbo 10 ambayo yana ushindani mkubwa.
Trump alimsifu Kennedy na kumtaja kama mtu wa “ajabu” na “mwerevu” wakati akimkaribisha jukwaani katika eneo la Glendale. Mpinzani wake wa chama cha Democrats Kamala Harris alisema angejaribu kupata uungwaji mkono wa wafuasi wa Kennedy.
Kennedy ni mtoto wa Seneta wa zamani wa Marekani Robert F Kennedy na ni mpwa wa rais wa zamani John F Kennedy, akitokea familia yenye ushawishi mkubwa katika siasa za chama cha Democrats.
Trump aliahidi kuwa iwapo atachaguliwa tena, angefichua kwa umma nyaraka zote zilizosalia kuhusu mauaji ya rais Kennedy ya mwaka 1963.
Lakini uamuzi wa Bw Kennedy wa kumuunga mkono mgombwa wa chama cha Republican umeghadhabisha jamaa na familia yake, ambao mnamo Februari walikosoa hatua yake ya kutumia jina la familia hiyo katika tangazo katika shindano la Super Bowl.
Kerry Kennedy, ambaye ni dada yake, alisema kwamba hatua ya kumuunga mkono Trump ni “kusaliti maadili ambayo baba yetu na familia yetu inachukulia kwa thamani kubwa. Huku ni kumalizika vibaya kwa hadithi mbaya.”
“Uamuzi huu unaniumiza sana kwasababu ya ugumu ambao umemsababishia mke na watoto wangu na marafiki zangu,” Bw Kennedy alisema siku ya Ijumaa.