Bilionea kutoka Afrika Kusini, Johann Rupert, amemshinda Aliko Dangote wa Nigeria katika orodha ya watu matajiri zaidi barani Afrika, kulingana na takwimu mpya kutoka kwa Bloomberg Billionaires Index.
Rupert ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Richemont, moja ya makampuni makubwa ya bidhaa za kifahari duniani, likiwa na chapa maarufu kama Cartier na Montblanc.
Thamani ya mali ya Rupert imeongezeka kutoka dola bilioni 12.4 hadi hadi kufikia dola bilioni 14.3, hivyo thamani ya mali zake kupanda kwa dola bilioni 1.9 na kumweka katika nafasi ya 147 duniani, nafasi 12 mbele ya Dangote.
Thamani ya mali za Dangote imepungua kwa dola bilioni 1.7 mwaka huu, na sasa ni dola bilioni 13.4 kutoka dola 15.1. Kupungua kwa mali ya Dangote kunafichua changamoto za kiuchumi zinazokabili Nigeria, ambapo kampuni yake inafanya shughuli.
Tangu Rais Bola Tinubu alipoingia madarakani mwaka jana, ametekeleza mageuzi kadhaa ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuondoa ruzuku za mafuta, jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei, sasa zaidi ya asilimia 30. Tinubu alisema mageuzi haya yalikuwa muhimu kupunguza matumizi ya serikali na kuhamasisha ukuaji wa muda mrefu.
Kupungua kwa thamani ya naira kumepunguza sana mali ya Dangote, ambaye utajiri wake unategemea sana mali zilizohesabiwa kwa sarafu ya ndani. Bilionea huyo mwenye miaka 66 alijipatia utajiri wake katika sekta ya saruji na sukari, na mwaka jana alifungua kiwanda cha mafuta katika mji wa kiuchumi wa Lagos.
Kampuni ya Dangote pia imekumbana na matatizo kadhaa hivi karibuni kutokana na ucheleweshaji wa uzalishaji katika kiwanda chake cha mafuta. Ingawa alitajwa na jarida la Forbes mnamo Januari kama bilionea tajiri zaidi Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya ugumu wa kiuchumi nchini Nigeria, orodha mpya ya Bloomberg sasa inamweka katika nafasi ya pili barani Afrika na 159 duniani.
Kufuatia kuongezeka kwa thamani ya mali ya Rupert, Nicky Oppenheimer, bilionea mwingine kutoka Afrika Kusini, ameshikilia nafasi ya tatu kwa utajiri barani Afrika akiwa na thamani ya dola bilioni 11.3. Mfanya biashara kutoka Misri, Nassef Sawiris, anashikilia nafasi ya nne kwa utajiri wa dola bilioni 9.48, huku mwekezaji wa Afrika Kusini, Natie Kirsh, akikamilisha orodha ya tano bora kwa utajiri wa dola bilioni 9.22.
Orodha ya Bloomberg, inafuatilia mabadiliko ya kila siku katika thamani ya mali ya watu matajiri zaidi duniani kama vile Forbes inavyofanya, na hivyo jina la tajiri zaidi barani Afrika linaweza kubadilika kulingana na hali ya soko na changamoto za biashara.