Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuokoa maisha yao kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ambayo itawaepusha na madhara yanayotokana na Nishati isiyo safi ikiwemo athari katika mfumo wa upumuaji.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Septemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla ya Azimio la Kizimkazi iliyolenga kuunga mkono jitihada za Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya Pika Kijanja inayoendeshwa na kituo cha redio cha Bongo Fm na Televisheni ya TBC.
Dkt. Biteko amesema, Rais Samia licha ya kuwa kinara wa Afrika kwenye kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia, pia amedhamiria kuwaondoa kina Mama na Baba Lishe wa Tanzania katika matumizi ya Nishati isiyo safi na pia kuboresha hali zao kwa kutumia Nishati safi ya Kupiki ambapo ametoa mitungi 2,000 kwa kundi hilo kama njia ya uhamasishaji wa nishati hiyo.
‘’ Nipende kumpongeza sana Mhe Rais kwa kuibeba ajenda hii ya Nishati safi ya Kupikia na kwa maono aliyonayo, nitoe agizo kwa Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha Wizara inashirikisha wadau kwenye kampeni hii ili iweze kufanyika kwa ufanisi na hivyo kumuunga mkono Mhe. Rais.” Amesema Dkt. Biteko
Akitoa takwimu za hali ilivyo kwa sasa, Dkt. Biteko amesema watu Bilioni 5.8 duniani ndio wanatumia Nishati Safi huku Bilioni 2.4 wakitumia Nishati isiyo safi ambapo Afrika Pekee ina watu milioni 933 wanaotumia Nishati isiyo safi na hivyo kuwataka wadau kuuganisha nguvu kuunga mkono matumizi ya Nishati iliyo safi.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Baba na Mama Lishe nchini na ndio mana kwenye hafla hiyo ya Azimio la Kizimkazi wamealikwa ili kuwahamasisha kuondokana na matumizi ya Nishati chafu na hivyo kuboresha mazingira yao ya ufanyaji kazi kwa kuwapatia Mitungi ya gesi kama Nishati mojawapo iliyo safi.
Alisema kimsingi muktadha wa Mhe Rais kama Kinara wa Nishati safi ya Kupikia Afrika ni utekelezaji pia wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza Watanzania kupatiwa Nishati Safi ya Kupikia kwa wakati na kwa gharama nafuu na ndio maana mitungi takriban 450,000 iliamuliwa iuzwe bei ya ruzuku ili kuwafikia wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambao ndio walioandaa kipindi cha Mhe. Rais cha Azimio la Kizimkazi, Bi Dafrosa Kimbori amesema TBC imeamua kuandaa kipindi hicho kupitia kampeni ya Pika Kijanja ili Rais Dkt. Samia awe mfano wa kuigwa na Watanzania katika kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji na uhamasishaji Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia na kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati ( Petroli na Gesi), Dkt. James Mataragio, Kamishna wa Umeme na Nishati jadidifu, Mha. Innocent Luoga, Wakurugenzi wa Taasisi chini ya Wizara ya Nishati, wadau wa Nishati ikiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Oryx na Total Energies ambao kwa pamoja wametoa mitungi 2,000 kwa Mama na Baba Lishe.