Wanawake wa Jamii ya Wafugaji (Masai) Wilayani Longido katika Mkoa wa Arusha wamejipanga kugombea nafasi za uongozi serikali za mtaa, kama ilivyo kwa wanaume tofauti na miaka ya nyuma iliyopita.
Akizungumza katika Kigoda cha mwanamke kwenye mfululizo wa mada za Wiki ya AZAKI Diwani Viti Maalum Tarafa Longido, Upendo Ndoros, amewataka Wanawake kuthubutu, na kuwa tayari kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu
Kwa upande wake Kiongozi wa mila wa jamii ya Kimasai Laigwanani Lucas Sambeke amesema wanawake wenye nafasi za uongozi ngazi ya jamii na hata serikali, wamefanya mabadiliko makubwa katika jamii hiyo na kuleta chachu ya maendeleo kwa ujumla.
“Kabla sijapata elimu kutoka Shirika la Legal Services Facility (LSF) nilijua mwanamke akiwa kiongozi atakuwa kiburi, dharau na kutotimiza wajibu wake kama mwanamke kwenye familia, lakini imekuwa tofauti na mtazamo wangu juu ya hilo” ameeleza na kuendelea,
“Kwa sasa mimi ni miongoni mwa viongozi wa mila wanaoshawishi jamii kumuamini mwanamke kupitia vikao na sherehe zetu, sababu nimeshuhudia wanavyobadilisha hali ya uchumi wa familia, kufanya maamuzi ya busara na kutetea haki za watoto na wanawake wengine, niko tayari kuwaunga mkono katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu” amesema Sambeke.
Afisa Maendeleo Wilayani Longido, Bi Nambori Nabak amepongeza namna mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanavyowapa wanawake elimu na mbinu za kujikwamua na umaskini, kupinga ukatili, na kupata nafasi za utawala kama ilivyo kwa wanaume.
“Nawashukuru sana Shirika la LSF, mmetufungua macho na kutupa ujasiri mkubwa, leo mimi nina hati miliki ya ardhi, ni kiongozi wa vikundi zaidi ya 300, na nimejua haki zangu, hii ni hatua kubwa na ninasema nitapigana usiku na mchana kuhakikisha wanawake tunapata nafasi za uongozi katika jamii yetu ili maamuzi yakifanyika maoni na mchango wa mwanamke uonekane” amefafanua Bi Nabak.
Sambamba na hayo Mtendaji wa kijiji cha Eworendeke Esupath Laizer amesema jamii inaendelea kubadilisha mtazamo juu ya mwanamke kwani mchango wake ni mkubwa na unaonekana licha ya majukumu makubwa aliyonayo.
“Sisi serikali tunaendelea kupiga vita ukeketaji na tumeunda kamati za siri zinazotupa taarifa, tunamuelimisha mwanamke namna ya kuzungumza na mwanae, kupinga mfumo dume na kutoa taarifa za ukatili na vitendo vingine vinavyokinzana na haki za mwanamke, pamoja na hayo tunahakikisha mtoto wa kike hakatishi masomo yake ili aweze kutimiza ndoto zake”
“Na katika jitihada zote za Serikali tunatambua mchango wa Asasi za Kiraia, mnatusaidia kuona mbali zaidi na kubadilisha maisha ya wananchi wengi” amesema Laizer.