Waziri wa afya, Jenista Mhagama amesema Wizara ya afya nchini itaendelea kuboresha huduma za afya kwa Watanzania ili kuifikia dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na kupata huduma bora ikiwemo matumizi ya Bima ya afya kwa wote.
Waziri Mhagama amesema hayo alipofanya ziara yake katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es salaam, lengo ikiwa ni kukagua na kuangalia hali ya utendaji kazi katika hospitali hiyo.
Amesema kuwa ili kuhakikisha huduma hizo zinanufaisha watanzania wizara hiyo itaimarisha usimamizi wa matumizi sahihi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo Bima ya afya kwa wote ili kuondokana na udanganyifu unaoweza kujitokeza.
Waziri Mhagama amesema uwepo wa matumizi ya Bima ya afya kwa wote itarahisisha ubora wa huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kupata matibabu kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI ), Dkt. Peter Kisenge,amesema katika kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi, hospitali hiyo inadhamiria kuimarisha teknolojia katika hospitali hiyo ili kufikisha huduma katika maeneo yote ya mjini na Vijijini.