DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya akina Mama na Uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Augustino Maufi, amewataka akina mama waliofikia umri wa kubeba mimba wenye changamoto ya Ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell), kufika mapema katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu.
Hayo ameyasema leo Septemba 18, 2024 wakati akitoa somo linalohusu Selimundu kwa akina mama wajawazito (Sickle Cell Anaemia in Pregnancy) kwa wauguzi na madaktari katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.
Dkt. Maufi ameeleza kuwa, kuna faida zaidi kwa mama kufika kituo cha afya ama hospitali mapema kabla hajabeba ujauzito ili kupewa elimu ya ushauri wa kitaalamu, lengo na dhumuni ni kulinda afya yake iweze kuishi na ugonjwa wa Selimundu.
“Tunajua Selimundu ni ugonjwa wa kurithi, tunashauri akina wakishafikisha umri wa kubeba mimba wafike hospitalini haraka ili tuje tuwashauri namna ya kuishi na ugonjwa huu.
“Katika kipindi cha ujauzito mabadiliko yanaweza kujitokeza muda wowote ikiwemo changamoto za ujauzito zinaweza sababisha ugonjwa selimundu kuwa tatizo kubwa”, amesema Dkt. Maufi.
Aidha, Maufi amebainisha athari ambazo zinaweza kumpata mama anayeishi na ugonjwa wa selimundu na endapo akichelewa kufika hospitali ni pamoja na kupata kifafa cha mimba inayosababisha na Shinikizo la Juu la Damu kutokana na ujauzito.
Vilevile, amesema mama anaweza kumbana na changamoto ya Kisukari cha Ujauzito, maumivu ya kifua, Oksijeni kushuka na hata maumivu ya mifupa.
Athari hizo zinaweza sababisha tatizo kubwa kwa afya ya mama na hata mtoto ikiwemo kifo kutokana na madhara ya ugonjwa huo ambao umesambaa zaidi kwa mikoa ya kanda ya ziwa.
Selimundu (Sickle Cell) ni Ugonjwa wa kurithi, unaotokana na uwepo wa seli za damu zenye umbo tofauti na la kawaida. Mtu mwenye tatizo hili huwa na changamoto ya kupungukiwa damu mara kwa mara, maumivu ya kichwa, viungo, pamoja na misuli.