Jeshi la Polisi linachunguza tukio la kifo cha Johnson Josephat maarufu kwa jina Sonii (39), mkazi wa Unga Limited jijini Arusha, aliyefariki dunia Septemba 23, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Justine Masejo amesema katika tarehe tajwa majira ya saa 11:30 jioni, Askari Polisi alifika katika maeneo ya Unga Limited kwa ajili ya kumkamata mtu huyo kuhusiana na tuhuma za kuvunja stoo na kuiba.
Amesema, wakati wa ukamataji Askari alifanikiwa kumvisha pingu mkono mmoja, ndipo lilipojitokeza kundi la watu na kumshambulia Askari kuzuia mtuhumiwa huyo asikamatwe na kufanikiwa kumtorosha kwa kutumia pikipiki.
SACP Masejo amebainisha kuwa taarifa za awali zinaeleza kuwa katika harakati za kumtorosha mtuhumiwa huyo, alianguka na baadaye ndugu walimfikisha Hospitalini.
Uchunguzi wa tukio hili unaendelea ili kubaini hasa nini kilisababisha kifo cha marehemu na wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Chanzo Dar24