Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameelezea dhamira ya Tanzania kwamba haifungamani na mkakati kutoka nchi moja katika kuendeleza Madini muhimu na Mkakati yanayopatikana nchini bali itashirikiana na Kampuni kutoka nchi yoyote duniani zitakazowekeza kwa kufuata misingi ya Sheria zinazosimamia Sekta ya Madini nchini
Dkt. Kiruswa aliyasema hayo jijini Las Vegas-Nevada Marekani wakati akishiriki kwenye mjadala wa madini umuhimu na mkakati katika uchumi wa madini kwenye maonesho ya Madini (MinExpo2024) yanayoendelea nchini humo.
Aidha, aliongeza kwamba, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini ikiwemo madini muhimu na mkakati yanaongezwa thamani hapa nchini ili kuinufaisha nchi kutokana na uwepo wa rasilimali hizo ambazo taifa limebarikiwa kuwa nazo
Dkt. Kiruswa alieleza kuhusu miradi mbalimbali ya madini mkakati inayoendelea nchini na kueleza kuwa hadi sasa kuna miradi 12 ambayo iko tayari kwa ajili ya kuendelezwa kuwa migodi huku sita ikihusisha madini ya kinywe (graphite).
Vilevile, ametumia jukwaa hilo kuelezea kuhusu mikakati ya Serikali kuendeleza madini mkakati ikiwemo kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia, na kuongeza kwamba ipo kwenye mchakato wa kuandaa Mkakati wa Madini Muhimu ambao kwa sasa uko kwenye hatua ya mashauriano na wadau.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa alitumia jukwaa hilo kuzikaribisha kampuni za utengenezaji wa vifaa na mitambo kutoka Marekani na nchi nyingine duniani zinazoshiriki katika maonesho hayo kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Novemba 19- 21, 2024 jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere na kueleza kuwa, wadau mbalimbali watafahamu kwa undani kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya madini nchini.
Dkt. Kiruswa ameambatana na wataalam kutoka Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)na wadau na kampuni mbalimbali kutoka Tanzania zikiwemo za uchimbaji na utoaji huduma migodini.
Chanzo Dar24