Watu watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka 23 likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na wizi wa fedha kiasi cha Shilingi 3,600,000.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Wangina Chacha (21), Erick Mushi (28), Shabani Msuya (36), Baraka Lunanja (32) na Kassim Dyamwale (34).
Wakili wa Serikali, Nitike Mwaisaka alidai hayo hapo jana Septemba 24, 2024 alipokuwa akiwasomea washtakiwa hao mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kemilembe Josiah washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani hapo.
Mwaisaka alidai katika mashtaka ya kwanza ya kuongoza genge la uhalifu na kuingilia mfumo wa kompyuta kwa lengo la kufanya uhalifu linawakabili washtakiwa wote ikiwa walitenda kosa hilo Julai, 28,2024 wakiwa katika maeneo ya Mabibo Mwisho, Wilaya ya Ubungo Dar es salaam.
Aliendelea kudai kuwa Julai 28, 2025 katika eneo la Mabibo Mwisho Wilaya ya Ubungo mshtakiwa namba mbili na tatu walijiwasilisha kuwa ni wafanyakazi huru wa kampuni wa mtandao wa simu Airtel kwa Wilbard Simon wakijua kuwa sio kweli.
Pia Julai 28, 2024 washtakiwa wote wakiwa katika eneo la Mabibo Mwisho, waliingilia mfumo wa kompyuta kinyume cha sheria kwa kutumia namba ya simu ambayo mmiliki ni Pius Mpanduli.
Alidai kuwa kosa la kutumia kifaa haramu na kuingilia mfumo kinyume na sheria linawakabili mshtakiwa namba moja, mbili, nne na tano, kati ya Septemba 8 hadi 11, 2024 washtakiwa walikutwa wana kifaa kilichoitwa “Screen recorder Unlimited”.
Washtakiwa hao walitenda kosa hilo wakiwa katika wilaya tofauti ndani ya Mkoa wa Dar es salaam na Tanga wakiwa wakitumia simu aina ya Infinix smart plus, Itel A05S, Samsung Galaxy A15, na Infinix smart 8.
Aliendelea kudai kuwa Julai 28,2024 washtakiwa wote wakiwa katika eneo la Mabibo Mwisho Wilaya ya Ubungo waliingilia akaunti ya Airtel Money inayomilikiwa na Paul Mpanduli kinyume cha sheria kwa lengo la kuiba.
Pia katika tarehe na eneo hilo washtakiwa wote waliiba fedha kiasi cha Sh 3,600,000 kutoka katika namba ya airtel inayomilikiwa na Paul Mpanduli.
Alidai mashtaka 11 ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine inawakabili mshtakiwa namba moja, mbili, tatu na tano, washtakiwa walidaiwa kufanya kosa hilo kati ya Julai 7, 2024 na Septemba 9, 2024 wakiwa katika maeneo tofauti ndani ya Mkoa wa Dar es salaam na Tanga.
Pia mashtaka ya mwisho yanawakabili washtakiwa wote watano, ilidaiwa kuwa Julai 28, 2024 wakiwa katika maeneo ya Mabibo Mwisho Wilaya ya Ubungo washtakiwa wote waliingilia data za kompyuta kinyume cha sheria kwa kuingilia mjumbe mfupi wa mfumo wa mawasiliano ya Pius Mpanduli.
Mwaisaka alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ambapo Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, 2024 na Washtakiwa wote walikosa dhamana na kurudishwa rumande.
Chanzo Dar24