Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali itapeleka Sh. Bilion 3.2 kwa ajili ya ujenzi w Kituo cha Afya, Shule ya Sekondari pamoja na barabara ya Lami Peramiho katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Peramiho.
“Mhe. Rais umenielekeza kutokana na idadi ya watu waliopo hapa Peramiho hawawezi kuendelea kupata huduma za Afya kwenye Zahanati hivyo Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilete Sh.Milioni 600 kwa ajili ya Kituo cha Afya, nikuahidi Mhe. Rais fedha zitaletwa mara moja ili ujenzi wa uweze kuanza,”amesema.
Aidha, amesema Mhe. Rais ameelekeza Sh. Milioni 600 zipelekwe kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari katika jimbo hilo.
“Nikuhakikishie Mhe. Rais kuwa fedha hizo zitaletwa mara moja ili watoto wa Peramiho waweze kusoma katika shule bora ya Sekondari, Serikali yako pia itaongeza mtandao wa barabara ya Lami yenye urefu wa Kilometa mbili ambao utagharimu takribani sh. Bilioni mbili,”amesema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo katika siku ya Pili ya ziara yake ya kikazi mkoani humo inayotarajiwa kuhitimishwa Septemba 28, 2024.
Chanzo OR-TAMISEMI