Guterres ameitoa kauli hiyo alipohutubia mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu uliofanyika mjini Baghdad nchini Iraq, baada ya Israel kutangaza mpango mpya wa operesheni kali zaidi katika ardhi ya Palestina iliyozingirwa.
“Tunahitaji usitishaji vita wa kudumu, sasa, nimeshtushwa na mipango iliyoripotiwa na Israel ya kutanua operesheni za kijeshi za ardhini, ” aliwaambia viongozi wa nchi za Kiarabu katika mkutano huo.
Viongozi hao wa nchi za Kiarabu wametoa pia wito wa kusitishwa mara moja kwa vita katika Ukanda wa Gaza , wakiishutumu vikali Israel kutokana na operesheni zake katika ardhi ya Palestina.
Wimbi jipya la mashambulizi ya Israel limesababisha vifo vya mamia ya watu tangu kusambaratika mwezi Machi, kwa makubaliano ya usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka. Siku ya Jumamosi, mamlaka za Gaza zimesema watu 146 waliuawa huko Gaza ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.
Ukosoaji katika mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu
Rais wa Misri Abdel-Fatah al-Sisi, ambaye nchi yake ni moja ya wapatanishi wakuu katika mazungumzo ya amani, ameikosoa Israel na kusema inafanya vitendo vya uhalifu katika ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alitoa wito wa kuiwekea Israel shinikizo zaidi ili kusitisha mauaji huko Gaza na kusema kuwa nchi yake inapanga kuwasilisha azimio la Umoja wa Mataifa litakaloitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kutoa uamuzi kuhusu mbinu za kivita zinazotumiwa na Israel.
Sanchez aliuambia mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Baghdad kwamba viongozi wa dunia wanapaswa “kuzidisha shinikizo kwa Israel ili isitishe mauaji huko Gaza, hasa kupitia mifumo na sheria za kimataifa”, akiongeza kuwa “idadi isiyokubalika” ya wahanga wa vita vya Israel na Hamas inakiuka “kanuni ya ubinadamu”.
Mazungumzo ya amani kufanyika mjini Doha, Qatar
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema kundi la wapiganaji wa Hamas limetangaza siku ya Jumamosi kwamba linajiandaa kurejea katika duru nyingine ya mazungumzo ya usitishaji wa mapigano itakayofanyika nchini Qatar.
Wakati huohuo Afisa mwandamizi wa Hamas amesema duru mpya ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Israel yenye lengo la kumaliza vita huko Gaza na “bila masharti yoyote” tayari yameanza mjini Doha siku ya Jumamosi.
Tangazo hilo limetolewa wakati jeshi la Israel likianzisha wimbi jipya la mashambulizi huko Gaza, likisema ni sehemu ya mpango mpya wa “kuvitanua vita katika Ukanda wa Gaza” likidai ni kwa lengo la kuwatokomeza wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas.
Wakati hali ya kibinaadamu ikizidi kuwa mbaya Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuepusha janga huko Gaza na kuiruhusu misaada kuingizwa na kusambazwa haraka eneo hilo. Umoja wa Mataifa umesema malori ya misaada karibu 9,000 yako tayari na yanasubiri ruhsa ya kuingia Gaza ili kuwasaidia maelfu ya Wapalestina waliopo kwenye hali mbaya.