Idadi hiyo ya vifo imetolewa na hospitali pamoja na maafisa wa afya kwenye Ukanda wa Gaza katika wakati Israel inatanua kampeni yake ya kijeshi kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.
Taarifa zinasema zaidi ya watu 48 wameuawa kwa mashambulizi ya anga ndani na pembezoni mwa mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis.
Baadhi ya makombora yalizipiga nyumba za makaazi ya raia na mengi yalianguka kwenye mahema yanayowahifadhi Wapalestina waliopoteza makaazi.
Miongoni mwa waliouawa ni watoto 18 na wanawake 13. Hayo yamefahamishwa na hospitali ya Nasser iliyopo kusini mwa Gaza.
Upande wa kaskazini mwa Gaza, shambulizi la Israel lililoilenga nyumba moja ndani ya kambi ya wakimbiri ya Jabalia imewaua watu 9 wa familia moja.
Wizara ya Afya ya Gaza, eneo linaloongozwa na kundi la Hamas, ndio imetoa taarifa hizo.
Idadi ya vifo yapindukia 400 ndani ya wiki moja
Shambulizi nyingine kwenye nyumba ya maakazi, nalo kwenye mji huo huo wa Jabalia, limeuwaua watu 10, wakiwemo watoto 7 na mwanamke mmoja.
Katika hatua nyingine maafisa wa afya wamesema mapigano karibu na hospitali ya eneo la kaskazini mwa Gaza na mzingiro uliowekwa na jeshi la Israel limesababisha hospitalo hiyo kufungwa.
Hospitali hiyo iitwayo Indonesia ilikuwa ndiyo pekee inayofanya kazi hivi sasa baada ya hospitali kubwa kwenye eneo hilo ya Kamal Adwan, kulazimishwa kuacha kuwahudumia Wapalestina mwaka jana kutokana na mashambulizi ya Israel.
Kwa jumla Wapalestina 464 wameuawa na jeshi la Israel katika kipindi cha juma moja lililopita.
Takwimu za wizara ya afya ya Palestina zimeonesha hivyo huku ikisema watu wengine 1,418 wamejeruhiwa kati ya Mei 11 hadi Mei 17.
Israel yatanua operesheni yake ya kijeshi Gaza
Jeshi la Israel halijasema chochote kuhusiana na hujuma hizo nzito zilizoanza tangu usiku wa manane kuamkia siku ya Jumapili.
Mara zote Israel imekuwa ikidai vifo vya raia wa Gaza vinasababisha na operesheni za Hamas ambayo inafanya kazi kwenye maeneo ya kiraia.
Mauaji hayo yanaripotiwa wakati israel inaongeza ukubwa wa operesheni yake ya kijeshi huko Gaza chini ya jina la “Giseon´s Chariots”.
Operesheni hiyo inajumuisha dhamira ya kuikopoka ardhi ya Gaza na kuwalazimisha mamia kwa maelfu ya Wapalestina kukimbilia kusini mwa ukanda huo.
Nchi hiyo pia imedhamiria kuchukua jukumu lote la usambazaji misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.
Utawala mjini Tel Aviv unadai kwamba kampeni hiyo mpya ya kijeshi inanuwia kuzidisha shinikizo kwa kundi la Hamas likubali usitishaji mapigano kwa muda chini ya masharti ya israel hatua itakayofungua njia ya kuachiwa mateka wote waliosalia wa Israel lakini hatomaliza vita.
Hamas yenyewe imesema inataka Israel iondoe kikamilifu vikosi vyake kutoka Gaza na kukomesha kabisa mashambulizi yake kwenye eneo kama sharti la kundi hilo kuridhia mkataba mpya wa kuacha mapigano.
Pande mbili zenye misimamo tofauti ya vita
Mkwamo kati ya pande hizo mbili umedhihirisha kuwa kihunzi kikubwa cha kumaliza mzozo huo uliopindukia miezi 19.
Wakati huo huo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema jopo lake la usuluhishi lipo nchini Qatar na linafanya kila linalowezekana kutafuta njia ya kupatikana mkataba wa kusitisha mapigano.
Ofisi hiyo imesema mkataba huo ni ule “utakaowarejesha nyumbani mateka 58 wa Israel waliosalia Gaza, kundi la Hamas liondoke kikamilifu kwenye ukanda huo na ardhi hiyo ya Palestina iwe eneo lisilo kabisa na silaha.”
Matakwa yote hayo yamepingwa vikali na Hamas ambayo imesema kamwe haitoichia ardhi ya Gaza wala kuweka chini silaha.