Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema Wizara yake imeendelea kutekeleza kikamilifu Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo ilizinduliwa Aprili 2023 na tayari imefikia mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Amesema Mkoa wa mwisho ambao ni Dar es Salaam, unatarajiwa kufikiwa Juni 2025 na Kwa upande wa Zanzibar, kampeni hiyo imekamilika katika mikoa yote mitatu
Dkt. Ndumbaro amezungumza hayo leo Mei 20, 2025 na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, akiweka bayana mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya sheria na haki nchini tangu kuanza kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amefafanua kuwa Kupitia kampeni hiyo, halmashauri 180, kata 1,907 na vijiji/mitaa 5,702 vilifikiwa, ambapo wananchi wapatao 2,698,908 walinufaika kwa kupata elimu na huduma za kisheria.
Aidha ameeleza kuwa idadi ya mashirika yanayotoa msaada wa kisheria imeongezeka kutoka 84 mwaka 2021 hadi 377 mwaka 2025, huku wasaidizi wa msaada huo wakiongezeka kutoka 617 hadi 2,205.
Pamoja na hayo amesema Serikali imeanzisha Madawati ya Msaada wa Kisheria katika mamlaka 184 za serikali za mitaa na kuwaajiri watumishi 449 ili kuyasimamia. Tangu kuanzishwa kwa madawati hayo, wananchi 6,427,738 wamepatiwa elimu ya sheria na haki za binadamu.
“Katika hatua ya kuimarisha utawala wa sheria, serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekamilisha uhakiki wa Sheria Kuu 300 kati ya 446 zilizotafsiriwa kwa Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu ya kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote, ” amesema
Waziri Ndumbaro pia ametangaza uwepo wa Kituo cha Huduma kwa Mteja kinachorahisisha upokeaji wa malalamiko kupitia njia mbalimbali ikiwemo simu, WhatsApp na barua pepe.
Amesema katika kipindi cha 2021 hadi 2025, idadi ya majaji imeongezeka kutoka 92 hadi 146 huku mahakimu wakiongezeka kutoka 1,412 hadi 1,426. Hali hii imechangia kupungua kwa mrundikano wa mashauri ambapo mashauri ya muda mrefu ni asilimia 4 pekee ya yote yaliyosalia mahakamani.
“Serikali imekamilisha ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika mikoa sita na inaendelea na ujenzi wa vituo vingine tisa. Mahakama za Wilaya na za Mwanzo pia zimejengwa na kukarabatiwa kwa kasi kubwa ili kuongeza upatikanaji wa haki kwa wote, ” ameeleza.
Vilevile amesema kuwa serikali imeongeza matumizi ya TEHAMA kwa asilimia 75 katika sekta ya sheria, na kuanzisha mifumo ya HAKI SHERIA na mfumo wa kutafsiri hukumu kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa kumbukumbu.
Ameongeza kuwa Ofisi za Mashtaka zimeongezeka kutoka 53 mwaka 2021 hadi 108 mwaka 2025. Katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, watoa huduma 498 wamesajiliwa hadi sasa.
“Kwa upande wa usajili wa watoto, zaidi ya watoto milioni 10 wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa tangu mwaka 2021, na Tanzania kutambuliwa kwa daraja “A” na taasisi ya kimataifa ya haki za binadamu kutokana na juhudi zake katika utawala bora, ” amesema.
Katika sekta ya elimu ya sheria, Waziri Ndumbaro amesema jumla ya wanafunzi 5,333 wamesajiliwa na 2,375 kuhitimu mafunzo ya uanasheria kwa vitendo tangu 2021. Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimehitimisha wanafunzi 2,876 katika ngazi ya cheti na astashahada.
“Mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha haki inatolewa kwa wote kwa haraka, kwa usawa na kwa gharama nafuu, huku akiendelea kuwahimiza wananchi kutumia huduma za kisheria zinazotolewa na serikali, ” amesema.