Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa taarifa ya kuonya dhidi ya kusambazwa kwa taarifa za uongo, za upotoshaji na zisizo na maadili kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), zikiwa zimewekewa nembo na jina la Jeshi hilo, na kuchapishwa kwenye ukurasa wa polisi, kwa nia ya kuuaminisha umma kuwa ndizo kauli rasmi za Polisi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mei 20, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi, DCP David Misime taarifa hizo ni za kughushi na hazijatolewa na Jeshi hilo.
“Taarifa hizo si za kweli na ifahamike kuwa Jeshi la Polisi haliwezi kuandaa na kusambaza taarifa kama hizo katika Mitandao yake ya kijamii,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Jeshi hilo limethibitisha kuwa limeanza uchunguzi kwa lengo la kuwatambua na kuwasaka wote waliohusika kuandaa na kusambaza taarifa hizo ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Wakati tunaendelea kufuatilia wahalifu waliotengeneza na kusambaza taarifa hizo ili wakamatwe, tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo na kuepuka kuendelea kuzisambaza endapo zitakufikia. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote yule aliyehusika na utengenezaji na utoaji wa tarifa hizo na yeyote yule ambaye ataendelea kuzisambaza.,” imeeleza taarifa hiyo.