Rais wa Marekani Donald Trump amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin amekuwa ‘mwendawazimu’ kutokana na kuendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Ukraine na ametishia kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi.
Akizungumza Jumapili, Trump amesema Putin amefanya mashambulizi ya anga ambayo yameilenga Ukraine na kusababisha mauaji ya takribani watu 13 wakati ambapo nchi hizo mbili zimebadilishana mamia ya wafungwa.
Trump ameandika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth kwamba siku zote amekuwa akisema Putin anaitaka Ukraine yote, na sio tu sehemu ya nchi hiyo.
Ameongeza kusema kuwa siku zote amekuwa na uhusiano mzuri na Putin, lakini kuna jambo limempata, kwani amekuwa mwendawazimu kabisa.
Trump asema Urusi inafanya mashambulizi bila sababu yoyote
Kulingana na Trump, wako katikakati ya mazungumzo, na Putin anawaua watu wengi bila sababu kwa kurusha makombora na droni katika miji ya Ukraine, bila sababu yoyote ile. Trump amesema hafurahishwi na jambo hilo na limemshangaza.
Hata hivyo, Rais Trump amemkosoa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa kutoitakia mema nchi yake, kutokana na jinsi anavyozungumza. Amesema Zelensky amekuwa akisababisha matatizo kutokana na matamshi yake, na bora aache kufanya hivyo. Trump amesema hivyo ni vita ambavyo visingeanza kama yeye angekuwa rais.
Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema huenda kauli ya Trump dhidi ya Rais Putin ilitokana na mihemko. Kulingana na Kremlin Putin amekuwa akiilinda Urusi. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amewaambia Jumatatu waandishi habari kuwa Putin anachukua maamuzi ambayo ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa nchi yake, akisema mashambulizi ya Urusi ni majibu ya mashambulizi yaliyofanywa na Ukraine.
Hata hivyo, hakuna majibu ambayo yametolewa hadi sasa na ofisi ya Zelensky kutokana na kauli ya Trump.
Trump azishinikiza Urusi na Ukraine kumaliza vita
Rais huyo wa Marekani amekuwa akizishinikiza Urusi na Ukraine kumaliza vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini pande hizo mbili hazina dalili ya kulifikia hilo, huku mataifa makubwa yakizungumza, vita vikiendelea na vikosi vya Urusi vinazidi kusonga mbele kuelekea mashariki ya Ukraine.
Wakati huo huo, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, ameyaelezea mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Ukraine kama “ya kutisha kabisa.”
”Ni wazi kwamba Urusi imeongeza shinikizo dhidi ya Ukraine. Ni kweli inaishambulia Ukraine kwa mabomu, tumeshuhudia mashambulizi mabaya zaidi. Kwa hiyo ni juu yetu kuweka shinikizo kwa Urusi ili nayo ikubali amani,” alifafanua mkuu huyo wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.
Kallas amesema wako tayari kutafuta amani kwa upande wa Ulaya, na wana matumaini kuwa washirika wengine wa kimataifa pia watafuata mkondo huo.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa kikosi cha anga cha Ukraine, Yuriy Ignat amesema Urusi imerusha droni 355 dhidi ya Ukraine usiku wa kuamkia Jumatatu, katika shambulizi kubwa kabisa tangu Urusi ilipovamia Ukraine mwaka 2022. Kwa mujibu wa Ignat, droni hizo zimerushwa ikiwa ni siku moja baada ya mashambulizi ya Urusi kuwaua watu 13.
Ukraine bado haijaripoti kuhusu vifo vilivyotokana na shambulizi la droni, lakini imesema kombora la Urusi lililorushwa ndani ya saa 24 zilizopita, limemuua mwanaume mmoja raia katika jimbo la Sumy, ambalo limekuwa chini ya mashambulizi ya Urusi kwa miezi kadhaa.