Jumla ya zaidi ya milioni 15 za madeni ya maji zimelipwa na wateja 287 katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, kufuatia ofa maalum ya msamaha wa faini iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ofa hiyo iliwalenga wateja waliokuwa wamekatiwa huduma ya maji na Mamlaka za Maji kote nchini, ikiwapa nafasi ya kurejeshewa huduma pasipo kutozwa faini na kuweka mpango maalum wa kulipa madeni yao kwa awamu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 2, 2025, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), Baby Lucas Biko, amesema tangu ofa hiyo ilipoanza kutekelezwa Mei 8 hadi Mei 31, 2025, jumla ya wateja 287 wameitikia wito huo na wamelipa zaidi ya Shilingi Milioni 15. Aidha, huduma ya maji kwao tayari imerejeshwa.
Ameongeza kuwa ofa kama hizi hutolewa mara kwa mara, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuzichangamkia pindi zinapotangazwa ili kuepuka usumbufu wa kukatiwa huduma.
Biko, amewahimiza wateja kulipa Ankara zao kwa hiari na kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya bili, ambayo huweza kusababisha kusitishiwa huduma na hatimaye kulazimika kulipa faini na gharama nyingine za kurejesha huduma hiyo muhimu.
Kwa upande mwingine, amebainisha kuwa kabla ya kutolewa kwa ofa hiyo, jumla ya wateja zaidi ya 2,400 walikuwa wamekatiwa huduma ya maji kutokana na madeni, baadhi yao sasa wameshalipa na kurejeshewa huduma huku wengine wakiendelea kufanya malipo kulingana na makubaliano waliyoingia na SOUWASA.
“Kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kunufaika na ofa ya Mei, bado tunaendelea kupokea maombi ya majadiliano ili kusaidia wateja wetu kurejeshewa huduma. Tunawahimiza wananchi kufuatilia na kuchangamkia fursa hizi pindi zinapojitokeza,” alihitimisha Biko.