Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limepokea tuzo ya heshima kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kudhibiti matukio ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu na jamii kwa ujumla.
Tuzo hiyo imekabidhiwa Leo (Juni 5, 2025), wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Walimu Wanawake na Walimu Wenye Ulemavu, uliohudhuriwa na walimu kutoka mikoa mbalimbali nchini. Mkutano huo ulilenga kuchagua viongozi wapya na kujadili masuala muhimu ya walimu.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Katabazi, alisema kuwa tuzo hiyo ni heshima kubwa na motisha katika kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii, hasa katika kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu.
“Jeshi la Polisi ni rafiki wa wote, lakini kwa yeyote atakayethubutu kuwadhuru walemavu au kufanya uhalifu kwa namna yoyote, atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Tunawahakikishia walimu kuwa wako salama mikononi mwa Jeshi la Polisi,” amesema Katabazi.
Pia aliwataka walimu kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu, ili kuhakikisha usalama wao wakiwa nyumbani au kazini. Alisisitiza kuwa ulinzi na usalama utatamalaki katika maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake, uongozi wa CWT ulieleza kuwa tuzo hiyo imetolewa kama ishara ya kuthamini ushirikiano mzuri uliopo kati ya walimu, wananchi, walemavu na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama, sambamba na kuwajali watu wenye uhitaji maalum.
Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga.