
Mahakama nchini Gabon, imemhukumu jela mke wa rais wa zamani Ali Bongo na mwanaye wa kiume, miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba fedha za umma.
Sylvia Bongo, na mwanaye Noureddin Bongo, wamepata kifungo hicho, baada ya kesi inayowakabili kufanyika kwa siku mbili.
Wakati wa kesi hiyo, wawili hao hawakuwa mahakamani, wakati waliposhtakiwa kumhadaa aliyekuwa rais Bongo, kuiba fedha za wananchi.
Viongozi wa mashtaka, waliwafungulia mashtaka wawili hao ambao wana uraia wa Ufaransa, kwa kushiriki kwenye kosa hilo, wakati kiongozi huyo wa zamani alipopata kiharusi mwaka 2018.
Hata hivyo, kiongozi wa zamani Ali Bongo aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 14 na baadaye kuondolewa madarakani na jeshi mwezi Agosti mwaka 2023, hajafunguliwa mashtaka.
Mbali na familia ya Bongo, waliokuwa washirika wake 10 nao pia wanakabiliwa na mashtaka ya kushiriki wizi wa fedha za umma katika kesi inayoendelea kusikilizwa hadi siku ya Ijumaa.
