
Nchini Uingereza, washirika wa karibu wa Waziri Mkuu Keir Starmer, wanasema, kiongozi huyo anapinga vikali mipango yoyote ya kujaribu kumwondoa madarakani.
Kauli hii imekuja, wakati huu kukiwa na hofu kuwa, kazi ya Waziri Mkuu Starmer, ipo hatarini, na hili huenda likashuhudiwa baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya serikali, wiki mbili zijazo.
Ripoti za ndani zinasema, kuwa washrika wa Waziri Mkuu Keir wana mashaka makubwa kuwa, kuna mpango ndani ya chama tawala cha Labour kumwondoa katika nafasi hiyo.
Baadhi ya vigogo wa chama hicho wanaotajwa kuwa huenda wakachukua nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa afya Wes Streeting na Waziri wa Mambo ya ndani Shabana Mahmood.
Kwa miezi kadhaa sasa, idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala cha Labour, wamekiri kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa serikali kupata mtikisiko mkubwa, baada ya uchaguzi wa majimbo huko Scotland na Wale, na ule wa serikali za mitaa katika baadhi ya maeneo nchini Uingereza mwezi Mei.
