
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazoanza kutumika kuanzia leo, Jumatano, Novemba 4, 2026, saa 6:01 usiku.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, bei za mafuta katika soko la dunia zilipungua kidogo mwezi Oktoba 2026 ikilinganishwa na mwezi Septemba, hata hivyo, bei hizo zimeendelea kuwa juu kutokana na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, ambako Tanzania hununua sehemu kubwa ya mafuta yake.
EWURA imeeleza kuwa ongezeko la gharama za usafirishaji na bima, pamoja na gharama za uagizaji wa mafuta, limechangia kuendelea kwa bei hizo kuwa juu.
Katika bei mpya zilizotangazwa, petroli kwa rejareja jijini Dar es Salaam itauzwa kwa Shilingi 4,083 kwa lita, dizeli Shilingi 4,128 na mafuta ya taa Shilingi 4,117.
Kwa upande wa Mkoa wa Tanga, petroli itauzwa kwa Shilingi 4,149 kwa lita, dizeli Shilingi 4,194 na mafuta ya taa Shilingi 4,183.
Mkoani Mtwara, petroli itauzwa kwa Shilingi 4,186 kwa lita, dizeli Shilingi 4,231 na mafuta ya taa Shilingi 4,220.
Aidha, EWURA imetangaza bei za jumla ambapo jijini Dar es Salaam petroli itauzwa kwa Shilingi 3,935.23 kwa lita, dizeli Shilingi 3,979.98 na mafuta ya taa Shilingi 3,969.83.
Mkoani Tanga, bei za jumla ni Shilingi 3,931.19 kwa lita ya petroli na Shilingi 3,974.06 kwa dizeli, huku Mtwara petroli ikiuzwa kwa Shilingi 3,930.70 na dizeli Shilingi 3,972.94 kwa lita.
Katika hatua nyingine, EWURA imeelekeza kuwa bei za rejareja za mafuta katika maeneo mbalimbali nchini zizingatie viwango vilivyoainishwa kwenye jedwali namba tatu la taarifa hiyo, huku wafanyabiashara wanaouza mafuta kwa jumla wakitakiwa kuzingatia bei zilizoainishwa kwenye jedwali namba mbili.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kukiuka agizo hilo.

