
Rais wa klabu ya Young Africans (Yanga), Eng. Hersi Said, amefunguka kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu klabu hiyo, ikiwemo mipango ya uwekezaji, maendeleo ya wachezaji vijana, mwenendo wa timu, malengo ya kimataifa pamoja na ujenzi wa miundombinu ya klabu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani, Hersi alisema uongozi umeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha Yanga inaimarisha ushindani wake na kujenga msingi wa mafanikio endelevu.
Katika mkutano huo, Hersi alieleza kuwa klabu imefanya tathmini ya mwenendo wa timu kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya michezo, ikiwemo kupoteza dhidi ya Simba na kutoka sare na TRA United, hali iliyosababisha kupoteza jumla ya pointi tano.
Alisema matokeo hayo hayakuwa matarajio ya uongozi wala mashabiki, hivyo klabu ililazimika kufanya maamuzi ya kiuongozi yaliyohusisha mabadiliko katika benchi la ufundi kwa kumaliza ushirikiano na kocha aliyekuwa akiongoza timu tangu mwanzoni mwa msimu.
Hersi alisisitiza kuwa pamoja na kutambua mchango wa kocha huyo, ikiwemo kuiongoza Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu itaendelea kufanya maamuzi magumu pale inapohitajika kwa maslahi mapana ya taasisi hiyo.
Katika eneo la maendeleo ya vijana, Hersi alisema Yanga imeendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wanaotoka katika timu zake za vijana kujiunga na kikosi cha wakubwa.
Alitolea mfano wachezaji KaziMoto na Saleh ambao wamepata nafasi ya kupanda kutoka katika timu za vijana na kujiunga na kikosi cha wakubwa, huku KaziMoto akionyesha maendeleo mazuri na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Aidha, alifichua kuwa klabu imeanza kupokea maombi kutoka kwa baadhi ya taasisi za soka za kimataifa zinazotaka kumpa nafasi mchezaji Abushiri maarufu kama Chuga kufanya majaribio.
Alisema Yanga ipo katika hatua nzuri za kukamilisha taratibu za kumwezesha mchezaji huyo kwenda nchini Brazil kufanya majaribio katika klabu ya Palmeiras, huku maandalizi ya nyaraka na visa yakiendelea.
Vilevile, mchezaji Saleh amepata fursa ya kwenda nchini Uingereza kufanya majaribio katika klabu moja ya soka, ambapo taratibu za safari yake zinaendelea.
Katika hatua nyingine, Hersi alieleza mafanikio ya programu ya Yanga Soccer School, akisema mpaka sasa wamepokea zaidi ya watoto 500 wanaopata mafunzo ya soka.
Alifafanua kuwa programu hiyo bado ni shule ya soka na haijafikia hatua ya kuwa akademi kamili, huku baadhi ya watoto wakigharamiwa na familia zao na wengine wakipata ufadhili kutoka kwa wadau mbalimbali.
Miongoni mwa wadau hao ni GSM Foundation inayofadhili watoto 30 na kampuni ya Emwani Coffee inayofadhili watoto 10.
UJENZI WA JENGO LA GHOROFA 13 KUANZA RASMI
Katika eneo la uwekezaji wa miundombinu, Hersi alitangaza kuwa ujenzi wa jengo la klabu lenye ghorofa 13 umeanza rasmi baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria, kiutendaji na kifedha kwa kushirikiana na Benki ya Azania.
Alisema benki hiyo imetoa mkopo utakaowezesha mradi huo kutekelezwa, huku fedha zikilipwa moja kwa moja kwa mkandarasi anayehusika na ujenzi.
Hersi alieleza kuwa mradi huo una changamoto za kihandisi kutokana na uwepo wa majengo makubwa jirani na eneo la ujenzi, hivyo wataalamu wamependekeza matumizi ya teknolojia ya Pile Foundation ili kuhakikisha jengo linapata msingi imara na shughuli za ujenzi zinafanyika kwa usalama.
Alisema mkandarasi tayari amefika eneo la mradi na kuanza maandalizi ya awali yanayojulikana kama Setting Out, huku hatua zinazofuata zikihusisha uchimbaji na uwekaji wa nguzo za msingi.
Kwa mujibu wa Hersi, jengo hilo litakuwa na ghorofa 13 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12, likiwa sehemu ya uwekezaji na mali za klabu ya Young Africans.
YANGA YALENGA ROBO FAINALI CAF CHAMPIONS LEAGUE
Kuhusu mashindano ya kimataifa, Hersi alisema Yanga imejiwekea lengo la kufika angalau hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026/2027.
Alisema klabu hiyo imeendelea kuweka historia kwa kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo mara nne mfululizo, mafanikio ambayo yamekuwa muhimu katika safari ya kuimarisha nafasi ya Yanga kwenye soka la Afrika.
Alikumbusha kuwa Yanga ilirejea hatua ya makundi mwaka 2023 baada ya kusubiri kwa miaka 25, tangu ilipofanya hivyo mwaka 1998.
Hata hivyo, alisema safari ya msimu huu haitakuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa katika kundi lao linalowakutanisha na Zamalek ya Misri, MC Alger ya Algeria na Club Africain ya Tunisia.
Hersi alisema wapinzani hao wana historia na uzoefu mkubwa katika mashindano ya Afrika, lakini Yanga inaamini katika uwezo wa kikosi chake na itapambana kuhakikisha inafikia malengo yaliyowekwa.
Alitaja mchezo dhidi ya MC Alger utakaochezwa Zanzibar Novemba 27 kuwa sehemu muhimu ya safari yao katika hatua ya makundi, huku kabla ya hapo wakitarajia kukutana na Polisi Tanzania katika Ligi Kuu ya NBC Novemba 20.
