
FLORIDA, MAREKANI: Mwanaume mmoja nchini Marekani, Doujon Duwayne Griffiths (26), amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua mwanamke aliyekuwa amemkaribisha nyumbani kwake pamoja na mtoto wake wa mwaka mmoja, huku pia akijaribu kumuua baba wa mtoto huyo.
Griffiths alihukumiwa Jumanne, Novemba 17, 2026, na mahakama nchini Florida, kufuatia mauaji yaliyotokea Septemba 7, 2021, katika eneo la Pine Castle, Florida.
Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Orange, Griffiths alipatikana na hatia ya mauaji ya Massania Malcolm na binti yake Jordania Malcolm, aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja, pamoja na kosa la kujaribu kumuua baba wa mtoto huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa Malcolm na mpenzi wake walikuwa wamemkaribisha Griffiths nyumbani kwao baada ya kubaini kuwa hakuwa na mahali pa kuishi. Hata hivyo, baadaye walizungumza naye kuhusu kutoshiriki gharama za maisha ya nyumbani na badala yake wakaamua kumsaidia kwa kumnunulia tiketi ya basi ili aweze kuondoka.
Inadaiwa kuwa tukio la mauaji lilitokea wakati familia hiyo ilipokuwa ikimpeleka Griffiths kituo cha mabasi. Katika mazingira ambayo hayajaelezwa kikamilifu, Griffiths alimpiga risasi baba wa mtoto huyo akiwa ndani ya gari.
Mwanaume huyo alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi kadhaa, lakini aliokolewa na kupelekwa hospitalini ambako alifanyiwa upasuaji.
Baada ya kushambuliwa, Malcolm alipatikana akiwa ameuawa kwa kupigwa risasi ndani ya gari, huku mtoto wake Jordania akifariki kutokana na joto kali lililokuwa ndani ya gari hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi, mtoto huyo aliachwa ndani ya gari na baadaye kufariki kutokana na athari za joto kali.
Griffiths hakukamatwa mara moja baada ya tukio hilo. Alifanikiwa kukwepa mkono wa sheria kwa kipindi cha takribani miaka mitatu kabla ya kukamatwa mwaka 2024 wakati wa ukaguzi wa kawaida wa gari katika eneo la Linden, jimbo la New Jersey.
Baba wa Jordania, ambaye ndiye aliyenusurika katika shambulio hilo, alikuwa shahidi muhimu katika uchunguzi na kesi iliyomkabili Griffiths.
Baada ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Jimbo la Florida, Monique Worrell, alisema kuwa Malcolm na mpenzi wake walimfungulia Griffiths milango ya nyumba yao wakati hakuwa na mahali pa kwenda, lakini aliwalipa kwa ukatili mkubwa.
Alisema familia imeachwa katika majonzi makubwa kutokana na kupoteza maisha ya watu wawili, wakiwemo mtoto mdogo ambaye ndiyo kwanza alikuwa ameanza kujifunza kutembea.
Kwa upande wake, Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Orange ilieleza kufarijika kutokana na hukumu hiyo, ikisema kuwa Griffiths sasa atatumia maisha yake yote gerezani kwa vitendo vyake vya kikatili.
Hata hivyo, pamoja na hukumu hiyo, familia ya marehemu Massania Malcolm na mtoto wake Jordania bado imebaki na maumivu ya kupoteza wapendwa wao katika mazingira ya kusikitisha.
