
Rais wa klabu ya Young Africans (Yanga), Eng. Hersi Said, amefunguka kwa kina kuhusu mchakato wa uwekezaji na ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, akieleza hatua mbalimbali za kiutawala, kisheria na kibiashara zilizofikiwa tangu kutangazwa kwa mpango wa kutafuta mshirika wa uwekezaji Januari 2026.
Hersi amesema Januari 7, 2026, Yanga ilitangaza rasmi kutafuta mwekezaji mshirika kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa uwanja, hatua iliyopokea maombi kutoka kwa taasisi mbalimbali kupitia Sekretarieti ya klabu.
Baada ya kupitia maombi hayo, klabu ilimtambua GSM Group kuwa mshirika anayefaa, kabla ya kutangazwa rasmi Februari 2, 2026, kufuatia kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Zanzibar.
Amesema makubaliano ya msingi kati ya pande hizo mbili yalikuwa kuanzisha kampuni maalumu ya kutekeleza mradi huo, inayojulikana kama Jangwani Complex Limited, kwa mfumo wa Special Purpose Vehicle (SPV).
Kupitia mfumo huo, Yanga inatarajiwa kuchangia ardhi kwa ajili ya mradi, huku GSM Group ikiingiza mtaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi, ambapo kila upande utamiliki asilimia 50 ya kampuni na mradi.
Hata hivyo, Hersi amefafanua kuwa kabla ya utekelezaji wa makubaliano hayo, klabu ilihitaji kupitia taratibu za kisheria kutokana na ukweli kwamba ardhi inayohusika ni mali ya klabu inayosimamiwa kupitia mfumo wa Baraza la Wadhamini.
Amesema Juni 9, 2026, klabu ilifanya kikao maalumu na Baraza la Wadhamini, ambacho kilihusisha pia ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, kwa lengo la kupata mwongozo kuhusu namna sahihi ya kisheria ya kutekeleza mradi huo.
Katika hatua nyingine, Hersi amesema Agosti 2, 2026, Yanga iliwasilisha suala la uhamishaji wa ardhi ya mradi kwa wanachama katika Mkutano Mkuu wa klabu, ambapo jumla ya wanachama 877 walihudhuria na kutoa ridhaa ya kuendelea na mchakato wa kuihamisha ardhi hiyo kwenda Jangwani Complex Limited.
Baada ya kupata ridhaa hiyo, klabu iliwasilisha nyaraka mbalimbali katika ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali kwa ajili ya tathmini na idhini, zikiwemo makubaliano ya uwekezaji, uthibitisho wa umiliki wa ardhi na kumbukumbu za vikao vya vyombo mbalimbali vya klabu.
Kwa mujibu wa Hersi, ucheleweshaji wa kuanza kwa ujenzi haukutokana na kukosekana kwa dhamira ya klabu, bali ulisababishwa na umuhimu wa kukamilisha taratibu za kisheria na kiutawala ili kulinda mali na maslahi ya wanachama.
Ameongeza kuwa katika kutafuta mfumo bora wa utekelezaji, Yanga ilipata nafasi ya kukutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na timu yake ya wataalamu, ambao waliwasilisha njia tatu zinazoweza kutumika katika kutekeleza mradi huo.
Tarehe 17 Novemba 2026, klabu ilipokea barua rasmi kutoka kwa Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali ikiwa na mwongozo kuhusu hatua zinazopaswa kufuatwa.
Baada ya kutathmini mapendekezo yote matatu, Kamati ya Utendaji na Baraza la Wadhamini zilikubaliana kuendelea na pendekezo la awali la kuhamisha ardhi ya mradi kwenda Jangwani Complex Limited.
Hata hivyo, Hersi amebainisha kuwa utekelezaji wa mfumo huo unapaswa kuzingatia ulinzi wa maslahi ya Yanga, GSM Group na wanachama wa klabu, hususan katika masuala ya umiliki na usimamizi wa mali.
Amesisitiza kuwa sehemu ya umiliki wa Yanga katika kampuni hiyo itaendelea kulindwa kupitia mfumo wa Baraza la Wadhamini na kwa kuzingatia taratibu zinazohusisha ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali.
Amesema lengo la klabu ni kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unakuwa na manufaa ya muda mrefu bila kuhatarisha haki za wanachama katika mali zao.
Hersi amewataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa na subira na kuendelea kuiunga mkono klabu, akisisitiza kuwa mradi huo ni muhimu katika historia ya taasisi hiyo na maendeleo ya soka la Tanzania.
Ameeleza kuwa uongozi utaendelea kushirikiana na mamlaka za Serikali pamoja na GSM Group kuhakikisha hatua zinazofuata zinakamilishwa kwa kuzingatia sheria na maslahi ya pande zote.
