KIUNGO wa Yanga, Salim Aboubhakar, ‘Sure Boy’ ameibukia ndani ya Mbeya kwa mara ya kwanza msimu wa 2022/23 akimpa mateso kipa wa Ligi Kuu Bara, Haroun Mandanda.
Sure Boy ndani ya msimu wa 2022/23 alikuwa hajafunga bao wala kutoa pasi ya bao katika mechi 21 ambazo alicheza na kutumia dakika 1,363 kuvuja jasho uwanjani akiwa na uzi wa Yanga.
Kaibuka Mbeya, Uwanja wa Sokoine akifanya kazi zote kwa wakati mmoja alipoingia akitokea benchi dakika ya 24 akichukua nafasi ya mshikaji wake Farid Mussa ambaye alipata maumivu kwenye mchezo huo.
Sure Boy bao lake la kwanza ndani ya Yanga alifunga dakika ya 68 akitumia pasi ya Khalid Aucho ikiwa ni baada ya kupitisha jumla ya dakika 1,402 bila kufunga na pasi yake ya bao aliitoa dakika ya 90 kwa Bernard Morrison ikiwa ni baada ya kukamilisha jumla ya dakika 1,429 alizotumia ndani ya Yanga.
Kiungo huyo anaingia kwenye orodha ya nyota waliotoka benchi na kubadili usomaji wa ubao wa Uwanja wa Sokoine baada ya dakika 90 kuwa Mbeya City 3-3 Yanga na kugawana pointi mojamoja.