Uwanja wa Jamhuri uliopo jijini Dodoma umeondolewa katika orodha ya viwanja vinavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025, baada ya kupoteza sifa zilizoainishwa kwenye kanuni na sheria za mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefanywa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya eneo la kuchezea (pitch) la uwanja huo kuonekana kukosa ubora ambapo sehemu kubwa haina majani ya kutosha na yaliyopo ni dhaifu jambo linaloufanya uwanja huo kutokuwa salama kwa wachezaji.
Taarifa ya leo Agosti 27, 2024 ya Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB imebainisha kuwa klabu ya Dodoma Jiji imetakiwa kupendekeza jina la uwanja mwingine miongoni mwa viwanja vilivyopitishwa kutumika kwa michezo ya Ligi, kwa ajili ya michezo yao ya nyumbani hadi pale uwanja wa Jamhuri utakapokuwa umefanyiwa maboresho ya kuondoa mapungufu yaliyoainishwa.
Aidha TPLB imezikumbusha klabu zote kuhakikisha zinaendelea kutunza miundombinu ya viwanja vyao katika kipindi chote cha msimu wa Ligi kwani kushindwa kufanya hivyo kutashusha ubora wa viwanja vyao na kusababisha viondolewe kwenye orodha ya viwanja vinavyotumika kwa michezo ya Ligi.