Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeshauri jamii kupenda kufanya mazoezi, kupunguza kula vyakula vya sukari, wanga na kusisitiza kwa wanywaji wa bia, kunywa angalau tatu kwa siku ili kujilinda na ugonjwa wa moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema hayo leo Jumatatu Julai 10, 2023 katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba).
Amesema kuna ongezeko la wagonjwa wa moyo nchini.
“Asilimia kubwa ya wanaolazwa hospitali ni wagonjwa wa moyo na shinikizo la damu,” amesema
Dk Kisenge ameshauri jamii kuzingatia kula lishe bora hasa mboga za majani na matunda, kupunguza vyakula vya wanga na sukari.
“Unywaji bia, angalau mnywaji anywe bia tatu kwa siku,” amesema
Mkurugenzi huyo amesema Watanzania wawe na kawaida ya kucheki afya zao mapema hii inasaidia kujijua na kupunguza madhara. Kwenye banda letu tunatoa huduma hizo na elimu ya afya ya moyo
Katika banda hilo pia wanatoa huduma ya tiba utalii ambayo imekuwa ikifanyika kwenye Taasisi na zaidi ya nchi 20 zimekwisha itembelea JKCI kufanya utalii huo wa matibabu.
“Taasisi ya JKCI imekuwa na uwekezaji wa vifaa vya upasuaji ambavyo unaweza kulinganisha na nchi yoyote kubwa duniani ambazo zinatoa huduma ya moyo.
“Tunapata watu mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi na hivi karibuni tulipokea watu kutoka Malawi waliokuja kuona huduma, kwenye maonyesho haya kuna nchi zaidi ya 47 hivyo tunayatumia pia kutoa huduma”
Mlele Mrisho Said ambaye ni miongoni mwa waliokwenda kupata huduma kwenye banda la JKCI amesema haikumchukua muda mrefu kupata huduma.
“Nilipewa maelekezo kwa dakika tano, kisha nikaenda kuwaona wahudumu kwa dakika tano, na kupanga foleni ya kuingia kwa daktari, huduma ni bure na baadhi unalipia kidogo sana, niliamua tu kuja kucheki afya na nimekuta presha imeshuka.”