Zaidi ya watu 300 waliokuwa wakisafiri kwa boti tatu za wahamiaji kutoka Senegal kwenda visiwa vya Canary nchini Hispania wamedaiwa kutoweka.
Kwa mujibu wa shirika la misaada la wahamiaji la Walking Borders la Hispani liliripoti tukio hilo la kutoweka jana Jumapili, Julai 9, 2023.
Shirika la Habari la Reuters, lilisema boti mbili za mwanzo ziliondoka nchini Senegal siku 15 zilizopita moja ikiwa na takriban watu 65 na nyingine ikiwa na watu kati ya 50 na 60.
Boti ya tatu iliondoka nchini humo Juni 27 ikiwa na takriban watu 200 ambapo jumla ni zaidi ya watu 300 ambao inataarifiwa wamepotea wakijaribu kufika nchini Uhispania.
Ofisa wa shirika la misaada la wahamiaji la Walking Borders la nchini humo, Helena Maleno alisema boti zote tatu ziliondoka mji wa pwani uitwao Kafountine kusini mwa Senegal, ambayo ni takriban kilomita 1,700 (maili 1,057) kutoka Tenerife, moja ya visiwa vya Canary.
“Familia zina wasiwasi mkubwa. Kuna takribani watu 300 kutoka eneo moja la Senegal. Wameondoka kwa sababu ya kukosekana kwa utulivu nchini humo,” alisema Maleno.
Inaelezwa visiwa vya Canary vilivyoko nchini Hispania ambapo ni karibu na Afrika Magharibi vimekuwa kivutio kikubwa cha wahamiaji wanaojaribu kufika nchini humo.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), takribani wahamiaji 559 walifariki dunia baharini mwaka jana wakijaribu kufika visiwa vya Hispania.
Shirika hilo linasema kwa mwaka 2021 idadi ya vifo ilikuwa watu 1,126.